NA GODFREY NNKO
AMIRI Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama nchini na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt.Samia Suluhu Hassan amesema,ulinzi na usalama wa Taifa upo salama na imara.
"Nchi yetu iko salama, mipaka yetu ipo salama na imara kwa sababu Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania limeendelea kutimiza ipasavyo jukumu lake la kulinda uhuru na mipaka ya nchi yetu."Rais Dkt.Samia ameyasema hayo Juni 27,2025 wakati wa hotuba ya kuhitimisha shughuli za Bunge la 12 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania jijini Dodoma.
"Jeshi letu la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania, lilitimiza miaka 60 tangu kuanzishwa kwake."
Amesema,katika kipindi hiki,Serikali imewekeza katika kuliimarisha kwa vifaa, zana za kisasa na mafunzo.
"Weledi na nidhamu ya Wanajeshi wetu ni ya hali ya kupigiwa mfano. Tumeboresha maslahi na makazi ya wanajeshi kwa kujenga nyumba mpya 6,064 za kuishi askari.
"Uwezeshaji huo umechangia kulifanya jeshi letu kushiriki ipasavyo katika shughuli mbalimbali za kitaifa na kimataifa, ikiwemo ulinzi wa rasilimali, ulinzi wa miradi mikubwa ya kimkakati, na oparesheni za ulinzi wa amani za Umoja wa Mataifa, hasa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Lebanon, Sudan Kusini na eneo la Abyei."
Kwa upande wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT),Rais Dkt.Samia amesema,wamepanua miundombinu na kuongeza idadi ya vijana wanaojiunga na jeshi kutoka 160,427 mwaka 2020 hadi 190,059 mwaka 2025.
Amesema,wamefanya hivyo kwa kutambua kuwa Jeshi la Kujenga Taifa ni nyenzo muhimu ya kujenga ujasiri, uzalendo na dhana ya kujitegemea miongoni mwa vijana.
Vilevile, SUMAJKT imeweza kushiriki kikamilifu kufanikisha utekelezaji wa miradi mbalimbali ya uzalishaji na miradi ya ujenzi.
Aidha, kwa upande wa Jeshi la Polisi,amesema wameendelea kuliimarisha kwa kuboresha mazingira ya kazi na kuongeza miundombinu, ambapo vituo vya polisi 472 vimejengwa hadi ngazi ya kata na shehia.
Halikadhalika,wameboresha makazi ya askari na kununua vitendea kazi, ikiwemo magari na pikipiki, kwa ajili ya kazi za utawala na operesheni.
Aidha,amesema askari wapya 16,009 wameajiriwa, huku Maofisa, Wakaguzi na Askari 10,363 wakipandishwa vyeo.
"Natoa pongezi nyingi kwa Jeshi la Polisi kwa kazi kubwa na nzuri wanayoifanya. Hatuna budi kutambua kwamba uhalifu unaozuiliwa kwa jitihada za Jeshi la Polisi ni mkubwa kuliko unaofanyika.
"Kasi ya kuwabaini na kuwakamata wahalifu, na kuwafikisha Mahakamani imeongezeka. Jambo ambalo bado hatujafanikiwa vya kutosha ni ajali za barabarani.
"Lazima nazo tuendelee kuzitafutia muarobaini wake. Aidha, nalielekeza Jeshi la Polisi kuongeza jitihada katika kukomesha matukio ya watu kupotea."
Pia,amesema Jeshi la Magereza nalo limeendelea kutekeleza vizuri majukumu yake ya kulinda wafungwa na kurekebisha tabia zao.
Aidha, katika kulinda haki za binadamu,amesema wameendelea kuboresha huduma za malazi, mavazi na chakula kwa wafungwa jinsi hali ya uchumi inavyoimarika.
Kwa upande wa watumishi, amesema Serikali imepandisha vyeo maafisa waandamizi na askari wa Jeshi hilo wapatao 14,733 na kuajiri askari wapya 3,404, hivyo kupunguza uhaba wa rasilimali watu.
Vilevile, amesema wamewapa vitendea kazi, ikiwemo magari kwa ajili ya kuimarisha utendaji kazi.
"Magereza mapya nane pamoja na Hospitali Kuu ya Kanda ya Jeshi la Magereza Dodoma, yanaendelea kujengwa."
Pia,amesema Serikali imewezesha jumla ya magereza 66 kuanza kutumia mfumo wa TEHAMA wa Mahakama Mtandao ambao unarahisisha usikilizaji wa kesi bila wafungwa kusafirishwa hadi mahakamani.
Mbali na hayo,ili kuongeza uwezo wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kufikia maeneo ya dharura kwa wakati,Rais Dkt.Samia amesema, Serikali imewezesha ujenzi wa vituo vipya vya zimamoto vitatu vilivyokamilika na vinane vinaendelea na ujenzi.
"Vilevile, vituo vya zamani vimefanyiwa ukarabati, na kununua magari 12 ya kuzima moto yakiwemo magari mawili yenye ngazi kwa ajili ya kufikia majengo marefu, na boti mbili za uokoaji katika Bahari na Ziwa Victoria."

Kwa upande wa Idara ya Uhamiaji,amesema zaidi ya maafisa, wakaguzi na askari 3,115 wamepandishwa vyeo, na askari wapya 2,251 wameajiriwa.
Aidha, doria, misako na operesheni ziliimarishwa katika maeneo mbalimbali nchini, na zimewezesha kukamatwa watu 97,538 kwa makosa ya uhamiaji, ambao wamechukuliwa hatua za kisheria, ikiwemo, kwa baadhi yao, kuondoshwa nchini.
"Vilevile, tunaendelea na ujenzi wa Chuo cha Mafunzo cha Uhamiaji cha Raphael Kubaga kilichopo Boma Kichakamiba Wilaya ya Mkinga Mkoani Tanga."


