ZANZIBAR-Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imesisitiza dhamira yake ya kuendelea kushirikiana kwa karibu na wataalamu wa fani za usanifu, uhandisi na ukadiriaji majengo katika utekelezaji wa miradi ya kimkakati inayoendelea nchini.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla, alitoa kauli hiyo wakati akimwakilisha Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, kwenye ufunguzi wa mkutano wa pili wa Taasisi ya Wasanifu, Wahandisi na Wakadiriaji Majengo Zanzibar (ZIQS), uliofanyika katika hoteli ya Verde, Mtoni.Alifahamisha kuwa serikali ya awamu ya nane imejikita ziadi kwenye miradi ya ujenzi, na hivyo kupatikana kwa fursa ya kushirikiana na wataalam wa fani hiyo katika kufanikisha miradi hiyo ya kimaendeleo.
Alisema ujenzi wa miradi hiyo unahitaji wataalamu waliobobea katika fani za uhandisi na ukadiriaji majengo, na kueleza kuwa serikali itaendelea kutoa kipaombelea kwa wakandarasi wazawa ili kutumia elimu na ujuzi walionao katika ujenzi wa nchi yao."Hii ni fursa kwa upande wenu. Muwe tayari kuichangamkia kwa kutoa utaalamu wenu katika miradi ya taifa," alisema Hemed.
Aliongeza kuwa serikali itaendelea kuwapa kipaumbele wakandarasi wazawa na kuwahimiza wawekezaji kuwatumia wataalamu wa ndani ili kukuza ujuzi na ajira kwa wananchi.
Kwa upande wake, Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Dk. Khalid Salum Muhammed, alieleza kuwa wizara yake itaendelea kusimamia wataalamu wa sekta ya ujenzi kwa kuhakikisha wanazingatia viwango vya kitaaluma na ubora katika utekelezaji wa miradi.
Rais wa Taasisi ya Wasanifu, Wahandisi na Wakadiriaji Majengo Zanzibar,mhandisi Abdul Samad Mattar, alisema mkutano huo umetoa fursa kwa viongozi na wanachama wa taasisi hiyo ya kujadili na kubadilishana utaalamu, ujuzi na uzoefu kwa lengo la kuhakikisha wanaendelea kufanya kazi kwa ubora na uweledi.







