ZANZIBAR-Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika Kongamano la Kwanza la Kitaaluma la Utumishi wa Umma, linaloandaliwa kwa pamoja na Chuo cha Utawala wa Umma (IPA) na Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC).
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika katika ukumbi wa Chuo cha Utawala wa Umma, Mkuu wa Chuo hicho, Dkt. Shaaban Mwinchum Suleiman, alisema kuwa kongamano hilo litafanyika Jumanne, tarehe 17 Juni 2025 katika ukumbi wa Hoteli ya Verde, Zanzibar.
Dkt. Shaaban alieleza kuwa kongamano hilo ni sehemu ya utekelezaji wa hati ya makubaliano ya ushirikiano baina ya vyuo hivyo viwili, ambayo inalenga kukuza elimu, taaluma, kufanya tafiti na kutoa huduma za ushauri elekezi kwa taasisi za umma na binafsi.
Amesema kuwa,Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, zimeendelea kuchukua hatua madhubuti katika kuboresha sekta ya utumishi wa umma kwa kuimarisha maslahi ya wafanyakazi, kufanya marekebisho ya sera na matumizi ya TEHAMA katika utoaji wa huduma za umma kwa uwazi, ufanisi na uwajibikaji.
Kwa mujibu wa Dkt. Shaaban, maudhui ya kongamano hilo ni "Mchango wa Uongozi, Teknolojia na Ubunifu katika Kuifikia Tanzania Imara", ambapo mada mbalimbali zitajadiliwa ikiwemo Uongozi wa Kimkakati kwa ajili ya kuimarisha Utawala Bora, Nafasi ya Ubunifu katika kuleta mabadiliko chanya kwenye Utumishi wa Umma, Matumizi ya Teknolojia katika kuimarisha utendaji kazi, uadilifu na uwajibikaji.
Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo na Mtendaji Mkuu wa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania, Dkt. Ernest Francis Mabonesho, alibainisha kuwa lengo kuu la kongamano ni kuwawezesha watumishi wa umma kuwa waadilifu, wawajibikaji na wenye kuzingatia maadili ya utumishi wa umma katika kuwahudumia wananchi.
Dkt. Mabonesho pia aliwahimiza waajiri kuwapeleka watumishi wao kwenye mafunzo ili kuwajengea uwezo na kuwawezesha kufanya kazi kwa weledi na kuendana na mabadiliko ya kiutendaji.
Kongamano hili linatarajiwa kuwahusisha washiriki 250 wakiwemo viongozi wa Serikali, wataalamu, wanataaluma na watumishi wa umma kutoka taasisi mbalimbali za Serikali
