SUZA, Jiangsu kushirikiana kuimarisha kilimo na ufugaji

ZANZIBAR-Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA),Prof. Moh’d Makame Haji amesema,chuo anachokiongoza kimefurahia kuanzisha uhusiano wa kitaaluma na Chuo cha Amali cha Jiangsu cha China kinachotoa taaluma ya masuala ya kilimo na ufugaji.
Kauli hiyo aliitoa wakati akiukaribisha ujumbe wa watu saba (7) kutoka Chuo cha Jiangsu uliofika makao makuu ya SUZA, Tunguu mkoa wa Kusini Unguja tarehe 11/06/2025.

Prof. Haji alisema ana imani kuwa uhusiano huo utaleta mafanikio kwa pande zote mbili hasa kutokana na kutoa taaluma zinazofanana.

Aliongeza kuwa SUZA inatoa umuhimu wa kipekee katika suala la uvuvi na Chuo kinatarajia kutoa mafunzo yanayohusiana na masuala ya bahari hivi karibuni.

‘’Chuo Kikuu kama chetu tuna jukumu la kuzalisha nguvu kazi ambayo itakuwa na uwezo wa kuajiriwa na kujiajiri kwa hivyo tuna furaha kwa uhusiano huu kuzidi kufanikisha malengo tuliyojiwekea’’, alisema Prof. Haji.

Mapema alisema, Mkurugenzi Mkuu wa Chuo Cha Amali cha Jiangusu, Bibi Cao Yumei alifahamisha kuwa Jimbo la Jiangsu lina vyuo vya Amali zaidi ya 2000 vinavyotoa taaluma mbali mbali hali iliyochangia kukua uchumi wa nchi.

Alifahamisha kuwa ufugaji wa kuku na kilimo ni miongoni mwa sekta zinazozalisha kwa wingi nchini China.

Aidha, vyuo 15 vya Amali katika jimbo la Jiangsu vimejenga uhusiano na vyuo na skuli 53 za Afrika hali inayochangia kubadilishana uzoefu na wataalamu mara kwa mara.

Hali kadhalika Bibi Cao aliahidi kukitangaza Chuo cha SUZA kujenga ushirikiano na vyuo vyengine vya China vinavyotoa taaluma zinazofanana ndani na nje ya nchi.

Katika mazungumzo hayo, washirika hao walikubaliana kuwa na ushirikiano katika masuala ya ubadilishanaji wa wataalamu wakiwemo walimu na wafanyakazi, kuimarisha mitaala ambayo itaendana na mabadiliko ya kisasa ya teknolojia sambamba na kukuza masuala ya kilimo na uchumi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news