MARA-Leo Juni 10, 2025 katika Mahakama ya Wilaya Tarime mkoani Mara mbele ya Hakimu Mfawidhi,Mheshimiwa Veronica Seleman imefunguliwa kesi ya Rushwa Namba 13960/2025 kati ya Jamhuri dhidi ya Tabibu wa Kituo cha Afya Magena,Jacob Ibrahim Wankyo.
Akisoma hati ya mashtaka, Mwendesha Mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU),Bw. William Lyamboko amedai, mshtakiwa huyo anashtakiwa kwa kosa la kuomba hongo ya shilingi 350,000 na kupokea hongo ya shilingi 200,000.
Ikiwa ni kosa chini ya kifungu cha 15(1)(a) na (2) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Sura ya 329 Pitio la 2022.
Bw. Wiliam Lyamboko alieleza kuwa, mshtakiwa huyo aliomba rushwa kwa mgonjwa aliyekuwa anatakiwa kufanyiwa upasuaji wa uzazi hivyo kuomba rushwa ili aweze kumpatia huduma hiyo ya upasuaji katika kituo hicho cha afya.
Hata hivyo, baada ya mshtakiwa kusomewa Hati ya Mashtaka amekana makosa yake.
Mshtakiwa amepata dhamana baada ya kutimiza masharti ya mahakama ambayo alitakiwa kuwa na wadhamini wawili ambapo kila mmoja alitakiwa kusaini fungu la dhamana ya shilingi 4,000,000.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Juni 26,2025 itakapokuja kwa ajili ya kusomwa kwa hoja za awali.