Tanzania na Rwanda zasaini makubaliano ya uimarishaji mpaka wa Kimataifa

NGARA-Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Rwanda zimetiliana saini makubaliano ya awali kwa ajili ya uandaaji wa Hati ya Makubaliano (MoU) kwa ajili ya uimarishaji mpaka wa Kimataifa baina ya nchi hizo.
Hatua hiyo imefikiwa Juni 12, 2025 mara baada ya kukamilika kwa Kikao cha Kamati ya Pamoja cha Wataalamu (JTC) kati ya Tanzania na Rwanda kilichofanyia katika mji wa Ngara Mkoa wa Kagera.

Utiaji saini huo umefanywa kati ya Mkurugenzi wa Upimaji na Ramani Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Bw. Hamdouny Mansour na Bw. Abel Buhungu ambaye ni kiongozi wa ujumbe kutoka nchini Rwanda.
Akizungunza mara baada ya utiaji saini makubaliano hayo, Bw. Hamdouny Mansour, ameshukuru kwa hatua iliyofikiwa ya kutiwa saini makubaliano ya uimarishaji mpaka wa kimataifa kati ya Tanzania na Rwanda na kueleza kuwa, ni matumaini yake maazimio yaliyofikiwa yatatekelezwa kama walivyokubaliana.

Naye kiongozi wa ujumbe wa Rwanda ambaye ni Mkuu wa Ubalozi wa Rwanda nchini Sudan, Mhe. Abel Buhungu ameshukuru serikali ya Tanzania kwa kuialika nchi yake kushiriki kikao cha pamoja cha uimarishaji mpaka wa kimataifa kwa nchi hizo mbili na kueleza kuwa, hana mashaka kwa kazi iliyofanyika na muda si mrefu watafikia malengo yaliyokusudiwa.
Wakati wa kikao cha JTC wajumbe walipata fursa ya kukagua mpaka wa wa kimataifa wa Tanzania na Rwanda ambapo ukaguzi ulianzia katika alama ya mpaka ya Mafiga Matatu (Kasange) mahali ambapo mto Kagera/Akagera unakutana na mto Mwidu kisha kuelekea Rusumo mahali ambapo mto kagera unakutana na mto Ruvuvu/Ruvubu.

Lengo la ukaguzi wa mpaka ni kubaini hali halisi ya mpaka ulivyo, maendelezo yanayoyafanyika na yale yaliyofanyika pamoja na shughuli za kibinadamu zinazofanyika.
Mpaka wa Tanzania na Rwanda una urefu wa takribani kilomita 230.

Zoezi la uimarishaji mipaka ya kimataifa ni utekelezaji wa makubaliano ya umoja wa Afrika kuwa ifikapo mwaka 2027 mipaka baina ya nchi za Afrika iwe imeimarishwa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news