Uchumi imara wa Tanzania waendelea kuvutia Kimataifa,Fitch yaipa Alama ya B+ na mtazamo thabiti

NEW YORK-Kampuni ya Kimataifa inayojihusisha na kufanya tathmini ya nchi kukopesheka katika masoko ya mitaji ya kimataifa ya Fitch Ratings, imeithibitisha Tanzania (Long-Term Foreign-Currency Issuer Default Rating – IDR) kuwa katika daraja la ‘B+’ ikiwa na Mtazamo Thabiti (Stable Outlook), jambo linalodhihirisha kuendelea kwa imani ya kimataifa juu ya misingi ya uchumi wa Tanzania na juhudi zake za mageuzi katika sera zake.
Kupitia taarifa yao waliyochapisha hivi karibuni, imesema uthibitisho huo umechangiwa na ukuaji imara wa Pato la Taifa (GDP), mfumuko mdogo wa bei, usimamizi mzuri wa sera za uchumi pamoja na kuimarisha ushirikiano na taasisi za kimataifa.

Kampuni ya Fitch inatarajia uchumi wa Tanzania utakua kwa asilimia 5.9 mwaka 2025, ukichochewa na sekta za kilimo, madini, utalii pamoja na uwekezaji katika miundombinu kama mradi wa reli ya kisasa (SGR) na mradi wa umeme wa Mwalimu Nyerere.

Tanzania imepongezwa kwa kudhibiti mfumuko wa bei, ambao umebaki ndani ya lengo la Benki Kuu ya Tanzania la asilimia 3 hadi 5, na kwa kuboresha usimamizi wa fedha za umma, ambapo madeni yaliyokuwa yakisubiri kulipwa kwa wazabuni na marejesho ya VAT yamepungua kutoka asilimia 1.2 ya GDP mwaka 2022 hadi asilimia 0.4 kufikia Machi 2025.

Fitch pia imeeleza kuwa kupitia matokeo hayo, wanatarajia mwelekeo wa sera kuendelea kuwa thabiti chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, jambo litakaloendelea kuwavutia washirika wa maendeleo na wawekezaji nchini.

Ripoti hiyo inaeleza pia kuwa, Tanzania imeweza kudumisha akiba ya fedha za kigeni, ambapo hadi Machi 2025 ilifikia Dola za Marekani bilioni 5.7, sawa na uwezo wa kulipia uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka nje kwa miezi 4.2.

Aidha, Fitch imeeleza kuwa kuongezeka kwa akiba ya fedha za kigeni, kuendeleza utekelezaji mzuri wa sera za uchumi na kuendelea kuvutia wawekezaji wa sekta binafsi kunaweza kuiwezesha Tanzania kupandishwa daraja zaidi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news