Zanzibar yapaa kiuchumi,Rais Dkt.Mwinyi asema huo ni mwanzo yanakuja mazuri zaidi

NA GODFREY NNKO

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt.Hussein Ali Mwinyi amesema kuwa, katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, uchumi wa Zanzibar umeimarika kwa kiasi cha kuridhisha ambapo hadi kufikia mwaka 2024, umekua kwa kasi ya asilimia 7.1.

Vilevile,Pato la Taifa kwa bei ya soko (GDP) nalo limeongezeka kufikia thamani ya shilingu trilioni 6.57 mwaka 2024 kutoka shilingi trilioni 4.78 mwaka 2021 sawa na ongezeko la asilimia 63.
Rais Dkt.Mwinyi Mwinyi ameyasema hayo leo Juni 23,2025 katika Ukumbi wa Baraza la Wawakilishi wakati akilihutubia Baraza la Kumi la Wawakilishi huko Chukwani Mkoa wa Mjini Magharibi, Zanzibar.

Pia,amesema Pato la mwananchi limeongezeka na kufikia shilingi milioni 3.22 mwaka 2024, sawa na Dola za Kimarekani 1,395 kutoka shilingi milioni 2.52 mwaka 2020 sawa na Dola za Kimarekani 1,099.
"Kadhalika, ukusanyaji wa mapato ya Serikali
umeongezeka kutoka shilingi bilioni 856 mwaka 2020/2021 hadi kufikia Shilingi trilioni 2.104 mwaka 2023/2024, sawa na ongezeko la shilingi trilioni 1.248."

Amesema,hali ya mfumko wa bei imekuwa ya kupanda na kushuka kutokana na kuongezeka kwa bei za bidhaa na huduma katika soko la Dunia.
Kwa Zanzibar,Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi amesema,kasi ya mfumko wa bei ilipungua hadi asilimia 5 kwa mwaka 2024.

"Tumeweza kudhibiti hali ya mfumko wa bei na kubaki katika tarakimu moja.Kwa lengo la kufanikisha utekelezaji mzuri wa mipango ya Serikali, bajeti ya Serikali imeongezeka kufikia shilingi trilioni 5.182.89 kwa mwaka wa
2024/2025 kutoka shilingi trilioni 1.579.2 kwa mwaka wa 2020/2021, sawa na ukuaji wa asilimia 228."

Aidha,Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi amesema, bajeti ya maendeleo imeongezeka kutoka shilingi bilioni 609.9 mwaka 2020/2021 na kufikia shilingi trilioni 3.271.11 kwa mwaka 2024/2025, sawa na ongezeko la asilimia 436.33.
Wakati huo huo,Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi amesema, kwa lengo la kuhakikisha wanakuwa na fedha za kutosha katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo, Serikali imeanzisha mpango wa Hati Fungani (SUKUK) inayofuata misingi ya sharia.

"Katika Awamu ya kwanza ya Mpango huu, Serikali imeweza kukusanya asilimia 128 ya lengo la makusanyo ya shilingi bilioni 300.
"Kwa mara nyengine, nitoe shukrani kwa wale wote waliojitokeza kuwekeza katika mpango huu muhimu wa SUKUK kwa maendeleo ya Zanzibar,"amesisitiza Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news