ZANZIBAR-Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Maji na Nishati Zanzibar (ZURA) imetangaza bei mpya za mafuta kwa mwezi Juni 2025, ambapo kumekuwa na punguzo la bei kwa bidhaa zote za mafuta.
Akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa ZURA, Meneja Uhusiano wa Mamlaka hiyo, Ndugu Mbarak Hassan Haji, amesema bei mpya zitaanza kutumika rasmi kuanzia Juni 9,2025.Amesema bei za mafuta kwa mwezi Juni 2025 kwa upande wa Petroli: Shilingi 2,968 kwa lita (kutoka 2,969), Dizeli: Shilingi 3,162 kwa lita (kutoka 3,191), Mafuta ya taa: Shilingi 3,150 kwa lita (kutoka 3,200), Mafuta ya ndege: Shilingi 2,521 kwa lita (kutoka 2,537).
Meneja huyo ameeleza kuwa upangaji wa bei hizo huzingatia vigezo mbalimbali vikiwemo wastani wa mabadiliko ya bei za mafuta katika soko la dunia, gharama za uingizaji kupitia Bandari ya Tanga, mabadiliko ya viwango vya fedha za kigeni, gharama za usafirishaji, bima, ada mbalimbali, pamoja na viwango vya faida kwa wauzaji wa jumla na rejareja.
Ameongeza kuwa, kupungua kwa bei katika mwezi huu kumechangiwa zaidi na mabadiliko chanya katika viwango vya kubadilisha fedha za kigeni kwa Shilingi ya Tanzania.
ZURA imewataka wananchi kununua mafuta katika vituo rasmi vinavyotambulika, na kudai risiti za kielektroniki kwa kila ununuzi ili kurahisisha upatikanaji wa huduma endapo changamoto zozote zitajitokeza.
Kwa mujibu wa utaratibu wake wa kawaida, ZURA hutangaza bei mpya za mafuta kila ifikapo tarehe 8 ya kila mwezi.