Aliyekuwa Mhasibu Msaidizi Kituo cha Afya Endagwe Babati afikishwa mahakamani kwa makosa ya rushwa na uhujumu uchumi

MANYARA-Juni 30,2025 katika Mahakama ya Wilaya ya Babati Mkoa wa Manyara limefunguliwa shauri la uhujumu uchumi namba 15921/2025.
Ni mbele ya Mheshimiwa Martin Masao, Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Mahakama ya Wilaya ya Babati dhidi ya aliyekuwa Mhasibu Msaidizi wa Kituo cha Afya cha Endagwe,Bw. Mohamed Twalib Baya.

Mshtakiwa anashtakiwa kwa kufanya ubadhirifu wa fedha kiasi cha shilingi 8,015,000 kinyume na kifungu cha 28(1) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Sura ya 329 kama ilivyorejewa mwaka 2022.

Pamoja na kuisababishia mamlaka hasara kinyume na Aya 10(1) katika jedwali la kwanza na vifungu vya 57(1) na 60(2) vya Sheria ya Uhujumu Uchumi na Makosa ya Kupangwa [Sura ya 200 Marejeo ya 2022].

Pia,ameshtakiwa kwa kosa la kughushi kinyume na kifungu cha 333, 335(a) na 337 vya Sheria ya Kanuni ya Adhabu Sura ya 16 marejeo ya 2022.

Mshtakiwa huyo amesomewa hati ya mashtaka na Mwendesha Mashtaka wa TAKUKURU,Bi. Neema Gembe akishirikiana na Bw. Davis Masambu na Bi. Catherine Ngessy.

Mshtakiwa amekana mashtaka yote yanayomkabili na shauri limeahirishwa hadi Julai 1,2025 kwa ajili ya masuala ya dhamana.

Kwa sasa mshtakiwa yupo mahabusu kwani ameshindwa kukidhi masharti ya dhamana.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news