MALABO-Katika mkutano wa Taasisi ya Maendeleo ya Umoja wa Afrika (AUDA-NEPAD) uliofanyika sambamba na Mkutano wa Umoja wa Afrika, viongozi kutoka kote barani wameahidi kuunda ushirikiano wa mageuzi na kufungua mikakati ya pamoja ya uhamasishaji rasilimali ili kutimiza malengo kabambe ya Ajenda ya 2063.
Mkutano huo, uliofunguliwa na Mhe. Mahmoud Ali Youssouf, Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika, wenye kaulimbiu ‘PAMOJA - Working Together to Ignite Regional Integration’ ulisisitiza umuhimu wa kuwa na juhudi za pamoja katika kushughulikia suala la ufanisi, kujenga uwezo, na ushirikishwaji wa diaspora ya Afrika.Mkutano huo umehudhuriwa na Bi. Nardos Bekele-Thomas, Mtendaji Mkuu wa AUDA-NEPAD, na Wajumbe wengine kutoka Taasisi za Umoja wa Afrika, na Jumuiya za Kiuchumi za Kikanda.
Pamoja na masuala mengine, vipaumbele muhimu vilivyotambuliwa ni kuoanisha mipango ya bara kuhusu uendelezaji wa viwanda, mabadiliko ya kidijitali, makabiliano ya mabadiliko ya tabianchi, pamoja na kuimarisha uwazi na uwajibikaji.
Jumuiya za Kiuchumi za Kikanda (RECs) na AUDA-NEPAD zilisititiza umuhimu wa kufanya shughuli zenye tija na matokeo hususani kutafuta fedha za ufadhili wa miradi ya kipaumbele zaidi ya 300 badala ya kuendelea na hulka ya kufanya mikutano kila mara.
Viongozi wamesisitiza juu ya utumiaji wa rasilimali za ndani, ushirikishwaji wa sekta binafsi, na uwezeshwaji wa wanawake kama moja ya vichocheo muhimu katika kufikia maendeleo endelevu. Aidha, viongozi walikazia kuwa suluhisho la matatizo yanalolikabili bara la Afrika ni jukumu la Waafrika wenyewe.
Kwa upande mwingine, Balozi Liberata Mulamula, Mjumbe Maalum wa Wanawake, Amani na Usalama wa Umoja wa Afrika amesisitiza Nchi kusaini na kuridhia Mkataba wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Wasichana.
Mkutano ulihitimishwa kwa dhamira ya dhati ya kuimarisha zaidi ushirikiano uliopo ili kujenga Afrika iliyo huru kifedha na yenye ustawi.














