DAR-Klabu ya Simba SC imetozwa faini ya shilingi milioni tatu kwa makosa matatu waliyoyafanya katika mchezo namba 184 wa Derby ya Kariakoo dhidi ya Yanga SC uliomalizika kwa Yanga Sc kushinda 2-0 katika dimba la Benjamin Mkapa mnamo Juni 25, 2025 jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa taarifa ya Julai 17, 2025 ya Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB), Simba SC imeadhibiwa kwa kutozwa faini ya shilingi milioni moja kwa kosa la kushindwa kuhudhuria mkutano wa wanahabari uliofanyika kwenye ukumbi wa Benki ya Taifa ya Biashara Dar es Salaam Juni 24, 2025 kinyume na matakwa ya Kanuni ya 17:58 ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo.
Katika hatua nyingine kikao cha Kamati ya TPLB kilichofanyika Julai 15, 2025 kimetoa uamuzi wa kuiadhibu Simba SC kwa kuitoza faini ya shilingi milioni moja kwa kosa la kushindwa kuhudhuria kikao cha kitaalam cha maandalizi ya mchezo (MCM) Juni 24, 2025 kinyume na matakwa ya Kanuni ya 17:2(2.2) ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo.
Pia,Simba SC imeadhibiwa kwa kutozwa faini ya milioni moja kwa kosa la kuingia kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa kupitia mlango usio rasmi kuelekea mchezo huo uliochezwa Juni 25, 2025.
Hiyo ikiwa ni kinyume na matakwa ya kanuni ya 17:21 ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo, adhabu ambazo zimetolewa kwa mujibu wa kanuni ya 17:62 ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo.
