MORONI-Benki ya CRDB imeendelea kuonesha dhamira ya dhati ya kupanua huduma zake ndani na nje ya mipaka ya Tanzania, kwa kuanza mchakato wa awali wa kutathmini fursa za uwekezaji nchini Comoro. Hatua inayoendana na mkakati wake wa kujitanua katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, ambapo kwa sasa inahudumia pia masoko ya Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

Ujumbe maalum kutoka Benki ya CRDB upo nchini Comoro kwa ajili ya kufanya upembuzi yakinifu kuhusu uwezekano wa kuanzisha kampuni tanzu katika taifa hilo, ikiwa ni sehemu ya maono ya benki hiyo ya kuimarisha ujumuishaji wa kifedha na kuchangia maendeleo ya kiuchumi ya kikanda.
Ziara hii imefanyika kufuatia wito wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, alioutoa tarehe 6 Julai 2025 katika maadhimisho ya miaka 50 ya Uhuru wa Comoro, ambapo aliwahimiza wadau wa sekta ya fedha kuangazia fursa za kibiashara na uwekezaji zilizopo nchini humo.
Ujumbe wa CRDB, unaoongozwa na Mkurugenzi wa Udhibiti wa Viashiria Hatarishi kutoka Makao Makuu ya Benki hiyo, Bw. James Mabula, umefanya mazungumzo rasmi na Balozi wa Tanzania nchini Comoro Mheshimiwa Said Yakubu.
Katika mazungumzo hayo, Mhe. Balozi Yakubu aliwasilisha taarifa ya kina kuhusu mazingira ya kijamii, kisiasa, na kiuchumi sambamba na hali ya uwekezaji nchini Comoro, ambayo imesaidia kujenga uelewa mpana kwa ujumbe wa CRDB kuhusu mazingira ya ndani ya nchi hiyo.
Wakiwa nchini Comoro, ujumbe huo umekutana na kuzungumza na Gavana wa Benki Kuu ya Comoro, Dkt. Younoussa Imani na ujumbe wake ambapo walieleza utambulisho wa benki hiyo, dhamira ya kushirikiana na taasisi za kifedha za Comoro ili kutoa huduma bora, jumuishi na bunifu kwa wananchi wa Comoro, ikiwa ni sehemu ya mchango wa benki hiyo katika kukuza uchumi wa Comoro.
Gavana wa Benki Kuu ya Comoro, Dkt. Imani, aliikaribisha kwa mikono miwili nia ya benki ya CRDB ya kuwekeza nchini humo na akaahidi kuipa ushirikiano ili kuhakikisha mchakato wa uwekezaji unafanyika kwa mafanikio na kwa kuzingatia misingi ya usimamizi bora wa sekta ya fedha.
Hatua hii ya CRDB si tu kwamba inaakisi mwitikio wa haraka na wa vitendo kwa wito wa Mheshimiwa Rais Samia, bali pia inaonesha msimamo thabiti wa benki hiyo katika kuwa mshiriki hai katika kukuza uchumi wa kikanda kupitia huduma bora za kifedha, zenye kuzingatia usawa, ujumuishaji na maendeleo endelevu kwa wananchi wa Afrika.










