Dkt.Hassy Kitine afariki

DAR-Aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa (TISS), Mbunge wa Makete, na Waziri wa Nchi-Ofisi ya Rais (Usalama wa Taifa),Dkt.Hassy Kitine amefariki dunia.

Kwa mujibu wa familia, maziko yake yanatarajiwa kufanyika kesho katika makaburi ya Kisutu jijini Dar es Salaam.

Dkt.Kitine alizaliwa mwaka 1943 katika Kijiji cha Kisinga, Makete. Alipata Shahada ya Uzamivu (PhD) nchini Canada alikoishi kwa takribani miaka 15, pia akihudumu kama Afisa Ubalozi wa Tanzania.

Aliwahi kujiunga na JWTZ na kupanda hadi cheo cha Kanali, kabla ya kuteuliwa na Rais na Amiri Jeshi Mkuu, Hayati Mwalimu Julius Nyerere kuwa Mkurugenzi Mkuu wa ldara ya Usalama wa Taifa Tanzania kuanzia mwaka 1978 hadi mwaka 1980.

Alijulikana kuwa mshauri wa karibu wa Mwalimu Nyerere, na ndiye aliyependekeza jina la Benjamin Mkapa kugombea urais mwaka 1995.

Katika utumishi wa umma, Kitine aliteuliwa kuwa Waziri wa Afya na baadaye Waziri wa Nchi-Usalama wa Taifa.

Akiwa mbunge, alitoa kauli kali dhidi ya rushwa na kudai kurejeshwa kwa maadili ya uongozi. Mwaka 2015, alitangaza nia ya kugombea urais kupitia CCM, akisema:
“Nipe miaka mitano tu, nitairejesha Tanzania ya Mwalimu.”

Dkt.Kitine ameacha urithi mkubwa wa uzalendo, uongozi na ujasusi wa kizalendo ulioegemea misingi ya maadili, uwajibikaji na heshima kwa Katiba ya nchi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news