NA GODFREY NNKO
MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango amezindua Mfumo Mkuu Jumuishi wa Kibenki (iCBS) chini ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT).


Uzinduzi huo umefanyika leo Julai 30,2025 makao makuu ndogo ya BoT jijini Dar es Salaam huku ukiongozwa na kaulimbiu ya "Tunaongoza Mustakabali wa Teknolojia katika Benki Kuu za Afrika".
Mfumo huo ambao ni matokeo ya kazi nzuri iliyofanywa na wataalamu wa ndani wa Benki Kuu ya Tanzania kwa kushirikiana na wataalamu wengine hapa nchini unatarajiwa kuwa na matokeo chanya katika sekta ya fedha nchini.
Katika uzinduzi huo, Mheshimiwa Dkt.Mpango ameipongeza Benki Kuu ya Tanzania kwa ubunifu wa mifumo ya kidijitali ambayo amesema,ni hatua njema kwa ustawi wa sekta ya fedha nchini.
"Benki Kuu ya Tanzania ni taasisi nyeti ambayo ina mchango mkubwa sana kwa Taifa letu, imesimamia uchumi wa Taifa letu kwa viwango vya juu sana," amesema Dkt.Mpango huku akitolea mfano namna ambavyo BoT ilisimamia uchumi kikamilifu katika kipindi cha misukosuko ya kiuchumi duniani hususani wakati wa UVIKO-19.
Dkt.Mpango amasema, Benki Kuu ya Tanzania imekuwa taasisi ya kwanza Barani Afrika kuunda Mfumo Mkuu Jumuishi wa Kibenki ambapo jumla ya shilingi bilioni 81.32 zimeokolewa kwa kutumia wataalam wa ndani na kuongeza ufanisi wa Benki Kuu katika kusimamia ufanyikaji wa miamala pasipo vizuizi.
Aidha,ametoa rai kwa Benki Kuu ya Tanzania kuhakikisha wanadhibiti na kuchukua hatua stahiki kwa wimbi la wakopeshaji kupitia mitandao ya simu na kuhakikisha wananchi hawaendelei kutapeliwa.
Vilevile, ameipongeza BoT kwa kuendelea kutoa elimu ambayo kwa kiwango kikubwa imeweza kuwapa mwanga wananchi kuhusu masuala ya fedha na kupunguza malalamiko.
Aidha, amewapongeza wataalamu wazawa ambao wametengeneza mfumo wa iCBS ambao umefanya kazi kwa miezi nane bila changamoto yoyote hadi alipouzindua leo.
Dkt.Mpango amesema kuwa, mafanikio hayo yanathibitisha wazi kuwa, Watanzania wakiamua wanaweza tena kwa ustadi mkubwa.
Wakati huo huo, Dkt.Mpango amezitaka taasisi nyingine za umma kuiga mfano wa Benki Kuu ya Tanzania kwa kuwekeza katika mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kupitia wataalamu wa ndani.
Amesema, mfumo wa iCBS utawezesha kudhibiti taarifa za Taifa katika sekta ya fedha hususani katika kipindi hiki ambacho Dunia inapitia katika ushindani mkubwa wa teknolojia ambapo uaminifu kwa wataalamu wa nje upande wa teknolojia si wa kutegemewa.
Dkt.Mpango ameiagiza Benki Kuu ya Tanzania kwa kushirikiana na taasisi nyingine ikiwemo Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kusimamia kikamilifu mfumo huu wa iCBS na mifumo mingine ya malipo na kuilinda dhidi ya uhalifu wa mitandao.
Awali, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Bw.Emmanuel Tutuba amemshukuru Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuwawezesha ili kuhakikisha wanafanikisha mfumo huo.
Aidha, amesema mbali na mfumo wa iCBS, Dkt.Mpango amezindua Makumbusho ya Benki Kuu ya Tanzania na Maktaba ya Kidijitali ya Benki Kuu ya Tanzania ili kurahisisha upatikanaji wa taarifa na maarifa mbalimbali kutoka BoT.
Gavana Tutuba amesema, katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan uchumi wa Tanzania umeendelea kufanya vizuri kipindi chote huku ukiwa himilivu na imara.
Pia, amesema upande wa upatikanaji wa mikopo umeendelea kuimarika katika sekta binafsi nchini.
Aidha, amesema hadi kufikia Juni, mwaka huu 2025 maduka yenye leseni kwa ajili ya kutoa huduma ya fedha za kigeni yamefikia 174 nchini huku benki zikiwa ni 37.
Kwa upande wa akiba ya dhahabu safi iliyonuliwa na BoT ambayo ipo katika akiba yake, Gavana Tutuba amesema, hadi kufikia Julai 29, mwaka huu imenunua jumla ya tani 6.8.
Gavana Tutuba amesema kuwa, mfumo wa iCBS ulianza kuundwa mwaka 2021 ikiwa ni utekelezaji wa maagizo ya Rais Dkt.Samia ya kuzitaka taasisi za umma kuwa na mifumo inayosomana ambapo ulikamilika Septemba, 2024 na kuanza kutumika kwa majaribio kuanzia Novemba, mwaka 2024.
Gavana Tutuba amesema, tangu kipindi hicho hadi sasa mfumo huo katika kipindi cha majaribio haukuonesha tatizo lolote, hivyo uzinduzi wa mradi wa iCDS ni hatua kubwa kwa Taifa la Tanzania.
Amesema, mfumo wa iCBS umesaidia katika kukabiliana na changamoto mbalimbali na kuleta maboresho makubwa kwenye maeneo mengi ikiwemo utoaji wa taarifa sahihi za serikali na kwa wakati.
Vilevile utoaji wa taarifa za miamala, ufungaji wa hesabu kwenye akaunti za wateja, upatikanaji wa taarifa kwa wafadhili, uhaulishaji wa fedha na ukokotoaji wa riba za kibenki.
Pia, ameongeza kwamba, uchumi wa Tanzania umeendelea kuimarika, thamani ya shilingi ya Tanzania imeendelea kuimarika pamoja udhibiti wa mfumuko wa bei.
Gavana Tutuba amesema, hadi kufikia Juni 2025 akiba ya fedha za kigeni ilifikia jumla ya dola za Marekani bilioni 6.2 ikiwa ni kiasi cha juu zaidi kufikiwa hapa nchini.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Fedha, Mheshimiwa Hamad Chande amewapongeza wataalamu waliobuni mfumo huo huku akihimiza umakini na ulinzi wake, kwani wengi hawatafurahia uwepo wake.
"Siyo jambo la kawaida kwa mfumo huu kujenga sisi wenyewe. Hongereni sana, kazi ambayo mmeifanya kuunda mfumo huu jumuishi ni historia kwa Benki Kuu ya Tanzania na Serikali kwa ujumla."
Kwa upande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango Zanzibar, Mhe. Dkt. Saada Mkuya Salum ameipongeza Benki Kuu ya Tanzania kwa kubuni mfumo huo huku akisema, pia uongozi wa BoT umekuwa mstari wa mbele kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika masuala mbalimbali yahusuyo sekta ya fedha nchini.
Hafla hiyo imehudhuriwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango Zanzibar, Mhe. Dkt. Saada Mkuya Salum, Naibu Waziri wa Fedha, Mheshimiwa Hamad Chande kwa niaba ya Waziri wa Fedha, Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Jerry Slaa, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Fedha na Mipango Zanzibar, Dkt.Juma Malik Akili,manaibu katibu wakuu wa fedha,viongozi wa juu wa Benki Kuu, uongozi wa mradi wa iCDS chini ya Meneja mradi huo Ali Salum Ali, Wakurugenzi wa Benki Kuu na Mameneja,maafisa watendaji wakuu wa benki na wengineo.