Dkt.Yonazi awahimiza watumishi Ofisi ya Waziri Mkuu kuongeza bidii katika kutekeleza majukumu yao

DODOMA-Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Dkt. Jim Yonazi amewaasa Watumishi wa Ofisi ya Waziri Mkuu kuendelea kufanya kazi kwa bidii na weledi mkubwa katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku.
Ameyasema hayo Julai 29, 2025 wakati akifungua Mkutano na Watumishi wa Ofisi hiyo ambapo alisema kuwa ni muhimu kuwa na nidhamu ya kazi, kushirikiana na kuendelea kuwa wabunifu katika majukumu ya kila siku, na kuwakumbusha watumishi kuwa kazi wanazofanya zinagusa maisha ya mamilioni ya wananchi, hivyo ni wajibu wa kila mtumishi kuhakikisha anatoa huduma bora na kwa viwango vya juu.
“Pia, nawasihi kuendelea kujenga mshikamano miongoni mwenu. Tunaposhirikiana, tunajenga nguvu ya pamoja ambayo hakuna changamoto inayoweza kutuzuia. Nawaomba tuendelee kufanya kazi kwa bidii na kwa moyo mmoja. Kumbukeni kuwa, kila mchango wenu una thamani kubwa katika kufanikisha malengo ya Ofisi yetu na Taifa kwa ujumla,"amefafanua Dkt.Yonazi.

Katibu Mkuu Yonazi aliendelea kusema kuwa, katika kuboresha Ofisi hiyo kwa mwaka wa fedha 2025/2026, Ofisi imeendelea kuboresha mazingira ya kazi kwa kushughulikia changamoto zinazohusu mazingira ya kazi na maslahi ya wafanyakazi ikiwa ni pamoja na kukuza ubunifu katika utendaji kazi wa kila siku na kuimarisha mifumo bora zaidi ya kufuatilia maendeleo ya kazi na kuhakikisha kila mfanyakazi anawajibika ipasavyo kwa nafasi yake.
Katika Mkutano huo watumishi wataweza kupata Elimu kutoka kwa wataalam wa Mfuko wa Uwekezaji wa UTT kuhusu umuhimu wa kuwekeza, pamoja na mambo mengine pia watapewa elimu itakayowakumbusha masuala mbalimbali yanayohusu uzingatiaji wa maadili ya utumishi wa umma, masuala ya Afya hususan homa ya ini na magonjwa yasiyoambukizwa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news