Ernest Sungura kuongoza Mabaraza ya Habari Duniani

ARUSHA-Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania (MCT),Ernest Sungura amechaguliwa kuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mabaraza ya Habari Duniani (World Association of Press Councils-WAPC). Hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Julai 18,2025 jijini Arusha na Makamu wa Rais, Baraza la Habari Tanzania,Yussuf Khamis Yussuf.

Aidha, amechaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa Mabaraza ya Habari ya Afrika Mashariki (East Africa Press Councils-EAPC).

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Bw.Sungura amechaguliwa wakati wa Mkutano wa Pili wa Mabaraza Huru ya Habari Barani Afrika (NIMCA) uliofanyika Julai 14 hadi 17, 2025 jijini Arusha, Tanzania.

Ni baada ya kuongoza kwa mafanikio na kufanikisha mkutano mkubwa wa kimataifa wa Mtandao wa Mabaraza Huru ya Habari Afrika (NIMCA), mkutano uliovutia washiriki zaidi ya 500 kutoka katika mataifa mbalimbali.
Kuchaguliwa kwa Bw. Sungura katika nafasi hizi mbili muhimu kunaonesha wadau wa tasnia ya habari kutoka ndani na nje ya bara la Afrika wana imani na uongozi wake.

Akiwa Katibu Mkuu wa kwanza wa WAPC kutoka ukanda huu, na Makamu Mwenyekiti wa EAPC, Bw. Sungura anaiwakilisha Tanzania katika mchango wa kimataifa wa kuunda mustakabali wa uandishi wa habari na mabaraza ya habari barani Afrika na duniani kwa ujumla.

Atashirikiana na David Omwoyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Baraza la Habari Kenya (MCK), ambaye amechaguliwa kuwa Rais wa WAPC na pia anahudumu kama Mwenyekiti wa EAPC. Bw. Peter Okello kutoka Baraza la Habari Uganda amechaguliwa kuwa Katibu wa EAPC, na Bi. Habiba Alasow Mohamed kutoka Shirikisho la Waandishi wa Habari Somalia amechaguliwa kuwa Mhazini wa EAPC.
Aidha, Bw. Ali Hancerli kutoka Jamhuri ya Uturuki ya Cyprus ya Kaskazini ameteuliwa kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa WAPC. Makamu wa Pili wa Rais ni Bw. Kishor Shrestha kutoka Baraza la Habari la Nepal; huku Dkt. Tamer Ataburut wa Baraza la Habari la Uturuki akihudumu kama Mhazini wa WAPC.

Kabla ya kushika nafasi hizi, Bw. Sungura alikuwa Mwenyekiti wa Kwanza wa Mtandao wa Mabaraza Huru ya Habari Barani Afrika (NIMCA) kuanzia Mei 2024 hadi Julai 2025, ambako amejenga misingi na kuweka viwango kwa uongozi ujao.
Bw.Sungura amekabidhi uenyekiti wa NIMCA kwa Pathiswa Magopeni ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Habari la Afrika Kusini.

Bodi ya Wakurugenzi ya Baraza la Habari Tanzania inampongeza kwa dhati kushika wadhifa huo wa utendaji katika Umoja wa Mabaraza ya Habari Duniani kwa kuwa Bodi inaamini Bw. Sungura atatekeleza majukumu yake ya kimataifa na kuchangia uwepo wa sera na sheria rafiki kwa waandishi wa habari kwa mataifa wanachama wa WAPC katika misingi ya uwazi, ustahimilivu, na maadili thabiti ya uandishi wa habari.

Kuhusu WAPC

Umoja wa Mabaraza ya Habari Duniani ulihuishwa mwaka 2004. Ni jukwaa la kimataifa linaloendeleza viwango vya maadili, uhuru wa habari, na uandishi wa habari wenye uwajibikaji duniani kote.

Makao makuu ya Sekretarieti ya umoja huo ipo mjini Istanbul, Uturuki, ambako pia Mhazini wa WAPC anasimamia shughuli kuu za kiutawala na uratibu.

Kuhusu EAPC

Ni umoja wa Mabaraza ya Habari ya Afrika Mashariki ambao ulianzishwa mwaka 2023 kwa lengo la kuunganisha mabaraza ya habari ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na kuweka viwango vya pamoja vya usimamizi wa maudhui na udhibiti wa sekta ya habari.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news