Gavana Tutuba afanya ziara Ubalozi wa Tanzania nchini Malawi

LILONGWE-Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT),Bw. Emmanuel Tutuba amefanya ziara katika Ubalozi wa Tanzania nchini Malawi, uliopo jijini Lilongwe. Katika ziara hiyo, Gavana alipokelewa na Balozi wa Tanzania nchini humo, Mhe. Agnes Kayola.
Akizungumza wakati wa mapokezi hayo, Balozi Kayola alieleza kuwa, uhusiano baina ya Tanzania na Malawi unaendelea kuimarika, hususani katika eneo la biashara.

Alisisitiza kuwa kiwango cha biashara kati ya nchi hizo mbili kimeongezeka kutokana na juhudi za kukuza diplomasia ya uchumi, ambayo inalenga kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi baina ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).

Kwa upande wake, Gavana Tutuba alieleza kuwa sekta ya fedha nchini Tanzania inaendelea kuimarika, hali inayochangia kukua kwa uchumi wa nchi. 

Alibainisha kuwa utekelezaji thabiti ya sera za fedha pamoja na usimamizi mzuri wa uchumi umeifanya Tanzania kuwa sehemu salama na ya kuvutia kwa wawekezaji wa ndani na wa kimataifa.

Aidha, alimtaka Mhe. Balozi Kayola kuendelea kuhamasisha wawekezaji kutoka Malawi na nchi jirani kuja kuwekeza nchini Tanzania, akisisitiza kuwa mifumo ya uwekezaji iliyopo ni rafiki kwa maendeleo ya biashara na viwanda.

Naye Balozi Kayola alieleza kuwa nchini Malawi pia kuna fursa nyingi za uwekezaji, na hivyo kuwahimiza Watanzania kuchangamkia nafasi hizo ili kukuza ushirikiano wa kiuchumi kati ya nchi hizi mbili jirani.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news