Gavana Tutuba azindua utaratibu wa usimamizi binafsi taasisi ndogo za fedha

NA GODFREY NNKO

GAVANA wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Bw.Emmanuel Tutuba amezindua rasmi utaratibu wa usimamizi binafsi kwa taasisi za huduma ndogo za fedha za daraja la pili kati ya BoT na vyama vya watoa huduma ndogo za fedha nchini
Uzinduzi huo umefanyika leo Julai Mosi, 2025 katika makao makuu ndogo ya BoT jijini Dar es Salaam. Vyama vilivyoshiriki katika makubaliano hayo ni Shirikisho la Taasisi Ndogo za Fedha Tanzania (TAMFI) na Umoja wa watoa huduma ndogo za Fedha Tanzania (TAMIU).

Awali, Gavana Tutuba amebainisha kuwa, "Kwa hiyo ushirikiano huu ninaamini kabisa utatengeneza nguvu ya pamoja ambayo itaboresha maisha ya Watanzania wengi na kuchochea maendeleo jumuishi ya kiuchumi.
"Endapo kutakuwa na lolote ambalo linahitaji muongozo au mkono wa Benki Kuu, sisi tupo tayari, lakini niwaombe na ninyi muwe tayari kwa taasisi zote zitakazokuwa chini yenu."

Pia, Gavana Tutuba amevipongeza vyama vya TAMFI na TAMIU zikiwemo timu zote za Benki Kuu na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) kwa kuanzisha utaratibu huo wa usimamizi binafsi kwa watoa huduma ndogo za fedha Daraja la Pili.

“Sasa, ni wakati wa kutekeleza makubalino yetu kwa juhudi, maarifa na uadilifu. Sina shaka kwamba hayo yote mtayatimiza kama tulivyokubaliana.”
Gavana Tutuba amebainisha kuwa, wakiyafanyia kazi makubaliano hayo hususani kila mmoja kwa dhamira ya dhati itachagiza kuleta mtazamo chanya kwa sekta ndogo ya fedha nchini.

Pia, amesema hatua hiyo itawezesha sekta hiyo kupanua wigo ambapo mwisho wa siku watoa huduma hao watapanuka na kuhama kutoka sekta hiyo kufikia hadi kuwa benki kamili.

“Sekta ndogo, ninaamini kila moja inapoanzishwa inakuwa na malengo, jukumu letu sisi tulilokabidhiwa la kusimamia sekta nzima ya fedha ni kuendelea kuwalea ili sekta hizi ndogo zikue zifikie kiwango cha kuwa benki.
"Kwa hiyo, hata wale walioko kwenye micro-finance ninaamini kila mmoja ana malengo yake, ninaamini malengo yao siyo kuwadhulumu, siyo kutengeneza dhuluma kwa wananchi, siyo kuwavizia ili wawanyanganye na kuwapora fedha zao, siyo kutumia zile Collateral ili iwe kama kiashiria cha kushika kwa muda, lakini kwa lengo la baadae wazihamishie kwao au wawadhulumu kwa kufanya hivyo, ni kinyume na masharti ya kisekta kwa hiyo kila mmoja atimize wajibu wake kwa staha ili tuzifanye hizi huduma ndogo za fedha mbele ya safari ziendelee kukuwa."

Gavana Tutuba amesema, kila mmoja akitoa mikopo ya staha kwa wananchi, pia itawawezesha kupata riziki nzuri ambayo haifungamani na dhuluma yoyote.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Shirikisho la Taasisi Ndogo za Fedha Tanzania (TAMFI) Taifa, Bi.Devotha Minzi amesema kuwa,watoa huduma ndogo za fedha nchini, daraja la pili wanapokea jitihada hizo kwa mikono miwili kwani zina manufaa mengi.

"Shukrani zetu za dhati ni kwako wewe binafsi Mheshimiwa Gavana, lakini pia kwa uongozi mzima wa Benki Kuu kwa sababu utayari wenu kwa pamoja ndio umewezesha kitu hiki kufanyika."
Pia, Mwenyekiti huyo ameguswa na namna ambavyo Gavana Tutuba kila anapopata fursa ya kushiriki mikutano ya Kimataifa amekuwa akijifunza jambo jipya huko nje ili kuangalia namna ambavyo linaweza kutumika kwa ajili ya kuiendeleza sekta ndogo ya fedha nchini kwa manufaa makubwa.
Amesema, makubaliano ya leo baina ya watoa huduma ndogo za fedha katika kujisimamia inawapa ari na shauku ya kufanya kazi kwa bidii, weledi ili kuhakikisha Watanzania wananufaika kupitia huduma wanazotoa kwa ustawi wa maendeleo yao na Taifa kwa ujumla.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news