DODOMA-Serikali imesema kuwa, mafunzo ya uimarishaji mpaka wa kimataifa kati ya Tanzania na Burundi yanalenga kujenga uelewa wa pamoja kati ya wataalamu wa nchi hizo mbili.
Hayo yamebainishwa leo tarehe 22 Julai 2025 jijini Dodoma na Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhandisi, Anthony Sanga wakati akifungua mafunzo ya siku tano ya uimarishaji mpaka wa kimataifa kati ya Tanzania na Burundi.
Kwa mujibu wa Mhandisi Sanga, mafunzo hayo ya wataalamu wa nchi hizo pia yataharakisha kasi ya uimarishaji mpaka wa kimataifa kati ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Burundi.
Aidha, amesema kuwa baada ya mafunzo hayo, kazi ya uimarishaji mpaka itakamilika kwa wakati na kusisitiza kwamba mipaka ya kimataifa ipo na unapofanyika uimarishaji ni pale panapotokea uharibifu katika mipaka hiyoKiongozi wa ujumbe wa Jamhuri ya Burundi Bw. Niyonkuru Apollinaire amesema, mafunzo hayo yataharakisha uimarishaji mpaka wa Kimataifa kati ya nchi yake na Tanzania kwa lengo la kuzifanya alama za mpaka kuonekana kwa usahihi na kusisitiza kuwa, nchi hizo kwa sasa zinao ushirikiano mzuri.
Zoezi la uimarishaji mipaka ya kimataifa ni utekelezaji wa makubaliano ya umoja wa Afrika kuwa ifikapo mwaka 2027 mipaka baina ya nchi za Afrika iwe imeimarishwa.
Tanzania imepakana na nchi 10 ambazo ni Kenya, Uganda, Burundi, Rwanda, DRC, Zambia, Malawi, Msumbiji, Comoro na Shelisheli huku mipaka baina ya nchi hizo ikiwa imegawanyika katika sehemu mbili za nchi kavu na majini.





