MTWARA-Mwaka 2025 umejaa neema tele kwa wakazi wa mji wa Mangaka, mji uliopo jirani kabisa na Mto Ruvuma. Pamoja na ukaribu huo wakazi wa mji wameishi na upungufu kwa huduma ya maji safi na salama.
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo, Serikali ya India, imeleta mageuzi makubwa, na huduma ya majisafi sasa upatikanaji wake punde unakuwa asilimia 100 kwa wananchi amba oni wadau wakuu wa Serikali. Ni matumaini mapya yaliyochomoza kupitia mradi mkubwa wa majisafi wa miji 28 ambao hivi sasa utekelezaji umefika asilimia 78.
Ujenzi wa mtambo wa kutibu maji katika Mradi wa Maji wa Miji 28 eneo la mji wa Mangaka, Mtwara ukiendelea, ambapo ukikamilika utakuwa na uwezo wa kuchuja, kusafisha na kutibu maji kiasi cha lita milioni tano kwa siku Kwenda kwa wananchi.
Mradi huu mpya wa maji unaotekelezwa na serikali ni sehemu ya mradi mkubwa wa kimkakati wa maji katika miji 28 nchini, unaofanikishwa kwa mkopo wa masharti nafuu kupitia Benki ya EXIM ya nchini India.
Mkataba wa ujenzi wa mradi huu ulisainiwa tarehe 6 Juni 2022 mkoani Dodoma na kushuhudiwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na utekelezaji wake ulianza rasmi tarehe 11 Aprili 2023.
Kwa mji wa Mangaka, gharama ya Dola za Marekani milioni 16.38 zinatumika na mradi huu unatekelezwa na mkandarasi kutoka India, kampuni za M/s Afcon Infrastructure kwa kushirikiana na Vijeta Projects & Infrastructure, chini ya usimamizi wa kampuni ya M/s WAPCOS wakishirikiana na umoja wa kampuni za GSB, Upimark pamoja na Mhandisi Consultant.
Hadi sasa, Dola milioni 13.25 zimelipwa kwa mkandarasi anayetekeleza mradi huku kazi ikitarajiwa kukamilika mwaka 2025.
Mradi wa Mangaka ni zaidi ya neema mkoani Mtwara. Mradi utakuwa na uwezo wa kuhudumia zaidi ya wananchi elfu 81 katika mji wa Mangaka na wilaya ya Nanyumbu ikiwa ni pamoja na vijiji 14 vinavyopitiwa na bomba kuu, unahusisha ujenzi wa banio la maji (intake) lenye uwezo wa kuzalisha maji kiasi cha lita milioni 5.5 kwa siku kutoka chanzo cha uhakika cha mto Ruvuma, mtambo wa kutibu maji wa lita milioni tano kwa siku, bomba kuu la kilomita 68.6, tenki la lita milioni moja na mfumo wa usambazaji wa maji kwa wananchi wenye jumla ya kilomita 34.
Kwa sasa, ujenzi wa banio umefika asilimia 93, mtambo wa maji asilimia 86, bomba kuu asilimia 90, tenki asilimia 95, na mfumo wa usambazaji asilimia 10.
Mradi unatarajiwa kuanza hatua ya majaribio na baadhi ya maeneo kuanza kunufaika na huduma ya majisafi.
USHUHUDA WA WANANCHI KUHUSU HUDUMA YA MAJI
Bi. Mariam Nkurua mkazi wa kijiji cha Matimbeni, mjini Mangaka, anasema:
"Tulikuwa tunatembea zaidi ya kilomita tatu kutafuta maji ya kunywa na kwa matumizi mengine ya nyumbani pia watoto walikuwa wanachelewa kuhudhuria masomo kwasababu ya maji, na wengine hata kuugua maradhi mbalimbali kwa kutumia maji yasiyo kuwa na ubora unaotakiwa.
"Mradi huu unaotoa maji katika Mto Ruvuma umetuletea tumaini jipya la maisha bora tena ya kisasa na kuepuka kushambuliwa na wanyawa wa hatari mtoni.”
Naye Bi. Zena Chipaka ambaye anajihusisha na ujasiriamali wa mazao na bidhaa ndogo ndogo, kuhusu huduma ya majisafi anasema
"Nilikuwa natumia muda mrefu katika huduma ya maji zaidi ya muda ninaotumia kujiingizia kipato katika shughuli zangu za kila siku za kiuchumi.
"Natarajia sasa kupitia mradi huu wa maji, nitafunga bomba la maji nyumbani kwangu na nitajikita zaidi kwenye biashara ya mazao na duka ili kuongeza kipato cha familia yangu na kuleta ahueni kubwa kwa ndugu na jamaa zangu."
Kwa upande wake, wakati Makala hii inaandikwa Diwani wa Kata ya Mangaka, Bw. Ibrahim Kasembe, anasema
"Mradi huu si wa kawaida. Ni ukombozi kwa wananchi wote wa Mangaka. Kwa mara ya kwanza, tutapata huduma ya majisafi na salama ndani ya makazi yetu na Mji wote wa Mangaka sasa unaenda kupata huduma ya maji kwa asilimia 100, tena maji baridi.
Hatua hii Serikali yetu itabadilisha maisha, afya na maendeleo ya kijamii kwa kiwango kikubwa."
Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Masasi Nachingwea (MANAWASA), Bw. Kiula Kingu anaeleza kuwa mradi huu unaendelea kwa kasi na kazi nyingi zikiwa zimekamilika kwa kiwango kikubwa.
Mkurugenzi Kingu anaeleza kuwa uchunguzi wa udongo katika eneo la mradi umekamilika kwa asilimia 85, ujenzi wa banio (intake) umefikia asilimia 93, na ulazaji wa bomba la maji ghafi kutoka katika chanzo hadi kwenye kituo cha kutibu maji umefika asilimia 90.
Aidha, anafafanua kuwa ujenzi wa kituo cha kutibu maji umefika asilimia 86 ya utekelezaji, wakati ulazaji wa bomba la kusafirisha majisafi umefika asilimia 90.
Kwa upande wa ujenzi wa tanki la kuhifadhia maji, asilimia 95 ya kazi iliyopangwa imeshakamilika.
Pia, amefafanua kuwa kazi ya usambazaji wa bomba la maji kutoka katika tanki hadi mji wa Mangaka bado iko katika hatua ya awali na imefikia asilimia 10.
Mkurugenzi Kingu anabainisha kuwa mradi wa maji wa miji 28 katika mji wa Mangaka ukikamilika utaleta mapinduzi makubwa katika maendeleo ya jamii kwa kutoa kiwango cha upatikanaji wa huduma ya maji kwa kufika asilimia 100 katika mji wa Mangaka kutoka asilimia 27.
Hivyo, unatarajiwa kuleta mabadiliko makubwa katika maisha ya wananchi wa Mangaka na wilaya yote ya Nanyumbu.
Akisisitiza kuwa mradi ni wa kimkakati na kwamba MANAWASA imejipanga kumaliza changamoto ya huduma ya maji kwa zaidi ya wakazi elfu themanini.
"Wananchi wataweza kupata huduma ya maji katika makazi yao jambo ambalo litapunguza muda na nguvu nyingi waliyokuwa wakitumia kutafuta huduma hii ya msingi,”Mkurugenzi Kingu amefafanua.
Kupitia uongozi thabiti wa Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Tanzania inaendelea kuandika historia ya mafanikio katika Sekta ya Maji na kujulikana katika mataifa mengine duniani kwa kutoa huduma bora yam aji kwa jamii.
Mradi wa Mangaka ni ushuhuda hai wa dhamira ya Serikali kuboresha maisha ya wananchi kwa vitendo.
Kwa mara ya kwanza katika historia ya Mangaka, wananchi watasema kwa sauti kubwa: "Hatimaye, maji yamefika!" na kazi ya “kumtua mama ndoo ya maji kichwani” imetumia.