NA JAMES MWANAMYOTO
OR-TAMISEMI
WAZIRI Mchengerwa ameeleza azma ya Serikari ya Awamu ya Sita ya kuhakikisha Mfumo wa Ufundishaji Mubashara (live teaching) unaanza kutumika nchi nzima ili kumuwezesha mwalimu kutoka katika kituo kimoja kufundisha wanafunzi wengi kwa wakati mmoja wakiwa katika mikoa tofauti.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI Mhe. Mohamed Mchengerwa akizungumza na wanafunzi wa Shule ya Sekondari Kibaha, mara baada ya kuzindua majaribio ya Mfumo wa Ufundishaji Mubashara (live teaching) Februari 07, 2024.
Azma hiyo ya Serikali imeelezwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI Mhe. Mohamed Mchengerwa, alipofanya ziara ya kikazi ya kuhimiza uwajibikaji kwa walimu na wanafunzi wa Shule ya Sekondari Kibaha ambayo ina kituo (smart class) cha ufundishaji mubashara (live teaching).
Waziri Mchengerwa amesema, anatambua kuwa Kibaha Sekondari ni moja ya kituo kinachotegemewa kwa ajili ya ufundishaji mubashara kwani mwalimu anaweza kufundisha akiwa Kibaha Sekondari na wanafunzi nchi nzima wakaudhuria kipindi chake.
“Kibaha Sekondari ni lazima muendelee kutumia Mfumo wa Ufundishaji Mubashara kwani niliuzindua mwenyewe jijini Dodoma kwa kuiunganisha Kibaha Sekondari na Dodoma Sekondari na tulijionea namna mfumo unavyofanya kazi na sasa tunataka uende nchi nzima,” Mhe. Mchengerwa alisisitiza.
Baadhi ya walimu wa Shule ya Sekondari Kibaha wakimsikiliza Waziri Mchengerwa (hayupo pichani) alipofanya ziara ya kikazi ya kuhimiza uwajibikaji katika shule hiyo yenye kituo cha ufundishaji mubashara (live teaching).
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI Mhe. Mohamed Mchengerwa akizungumza na walimu wa Shule ya Sekondari Kibaha (hawapo pichani) alipofanya ziara ya kikazi ya kuhimiza uwajibikaji katika shule hiyo yenye kituo cha ufundishaji mubashara (live teaching).Sanjari na hiyo, Mhe. Mchengerwa amempongeza Mkurugenzi wa Manispaa ya Kibaha Dkt. Rogers Shemwelekwa kwa kuhimiza matumizi ya Mfumo wa Ufundishaji Mubashara katika Shule ya Sekondari Kibaha na kumtaka aendelee kuiwezesha shule hiyo kuwa kituo cha mfano cha ufundishaji mubashara nchini, kwani wakati akiwa Shirika la Elimu Kibaha aliwezesha mfumo huo kufanya kazi.
Waziri Mchengerwa amefafanua kuwa, iwapo miundombinu ya elimu itaendelea kuboreshwa katika Shule ya Sekondari Kibaha, hapo baadae kuna uwezekano Serikali ikafikiria kujenga chuo kikuu katika eneo hilo hilo ambalo shule hiyo ipo ili kutimiza lengo la Rais Samia la kuhakikisha kila mtanzania anapata elimu.
Aidha, Waziri Mchengerwa amempongeza Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari Kibaha Bw. George Kazi kwa kazi nzuri anayoifanya na kumtaka aendelee kuhakikisha wanafunzi wa kidato cha nne na cha sita wanaendeleza utamaduni wa kupata ufaulu mzuri, na kuongeza kuwa akishindwa kutekeleza jukumu hilo atawajibishwa.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI Mhe. Mohamed Mchengerwa akieleza umuhimu wa Mfumo wa Ufundishaji Mubashara kwa wanafunzi wa Shule ya Sekondari Dodoma, mara baada ya kuzindua majaribio ya mfumo huo (live teaching) Februari 07, 2024. Wanaoonekana kupitia mfumo huo ni wanafunzi wa Shule ya Sekondari Kibaha.Kwa upande wake, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari Kibaha Bw. George Kazi amemueleza Waziri Mchengerwa kuwa yeye pamoja timu nzima ya walimu anaowaongoza wamejipanga kuhakikisha wanaendelea kufundisha usiku na mchana ili kutoa ufaulu mzuri kwa wanafunzi wote wanaomaliza Kibaha Sekondari.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI Mhe. Mohamed Mchengerwa mnamo Februari 07, 2024 alizindua majaribio ya Ufundishaji Mubashara katika Shule ya Sekondari Dodoma, majaribio hayo yameonesha matokeo chanya katika kuongeza ufahamu wa wanafunzi kwenye shule ambazo zina vituo (smart classes) vya Ufundishaji Mubashara (live teaching).
