Mwandishi anayegombea nafasi ya kisiasa anapaswa kuondoka kwenye chumba cha habari-MCT

ARUSHA-Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, Ibara ya 21(1), inampa kila raia haki ya kugombea nafasi za kisiasa. Ibara hiyo inasema: "Kila raia wa Jamhuri ya Muungano anastahili kushiriki katika Serikali ya nchi hii, ama moja kwa moja au kwa kupitia wawakilishi waliochaguliwa kwa hiari yake, kwa kufuata utaratibu uliowekwa na Sheria."
Hayo yamebainishwa Julai 2,2025 na Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania (MCT),Ernest Sungura wakati akitoa mwongozo kwa wanachama,waandishi wa habari na umma wakati wa uchaguzi mkuu.

"Hii inajumuisha haki ya kupiga kura na kugombea katika chaguzi mbalimbali. Kwa hali hiyo, waandishi wa habari wana haki ya kugombea nafasi za kisiasa kama ilivyo kwa raia wengine.

"Hata hivyo, kuendelea kuwa mwandishi wa habari huku ukijihusisha na siasa ni kinyume cha maadili ya taaluma hii. Mwongozo unaelekeza kwamba mwandishi anayegombea nafasi ya kisiasa anapaswa kuondoka kwenye chumba cha habari ili kuepuka mgongano wa maslahi na kupoteza uaminifu wa umma.

"Waandishi wa habari wanaojihusisha na siasa kwa kugombea nafasi za uongozi huku wakiendelea na kazi yao wanakabiliwa na athari kubwa kwa taaluma yao na tasnia ya habari kwa ujumla.

"Kwanza, kuna suala la kupoteza uaminifu. Wananchi na vyombo vingine vya habari hawawezi kumwamini mwandishi ambaye anaegemea upande wa kisiasa, kwani taarifa zake zitaonekana kuwa na upendeleo au ajenda ya kisiasa badala ya ukweli na uwazi.

"Pili, kuna mgongano wa maslahi. Mwandishi hawezi kuripoti kwa haki na usawa akiwa ana maslahi binafsi katika uchaguzi, kwani anaweza kushawishika kuandika kwa faida yake au chama chake badala ya kuzingatia ukweli na maadili ya uandishi wa habari.

"Zaidi ya hayo, kuchanganya siasa na uandishi wa habari kunaharibu tasnia ya habari kwa kuifanya kuwa chombo cha propaganda badala ya kuwa chanzo cha taarifa sahihi. Hali hii inapunguza hadhi ya taaluma ya uandishi wa habari na kuathiri uwezo wa vyombo vya habari kutoa taarifa kwa uwazi na bila upendeleo.

"Kwa kuzingatia athari hizi, mwandishi wa habari anayegombea nafasi ya kisiasa anapaswa kujiondoa rasmi kwenye chumba cha habari ili kuepuka mgongano huo wa kimaslahi na kulinda uaminifu wa taaluma ya uandishi wa habari.

"Hata hivyo, mwandishi huyo iwapo atataka kurudi kwenye tasnia ya habari baada ya uchaguzi, anaweza kufanya hivyo kwa kuwa mwandishi wa makala maalum safu huku akiweka wazi katika makala yake kuwa aliwahi kugombea kupitia chama fulani cha siasa.

"Hatua hii inasaidia kulinda uwazi na kuzuia upotoshaji wa habari kwa wasomaji, huku taaluma ya uandishi wa habari ikibaki kuwa huru na yenye kuaminika;

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news