Mwenendo wa ukuaji wa uchumi wa Tanzania upo vizuri-BoT

NA GODFREY NNKO

MWENYEKITI wa Kamati ya Sera ya Fedha ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Bw. Emmamuel Tutuba amesema, ukuaji wa uchumi kwa Tanzania Bara unakadiriwa kufikia asilimia 5.8 katika robo ya kwanza na asilimia 5.5 katika robo ya pili ya mwaka 2025.

Vilevile, nakisi ya urari ya malipo ya kawaida ilipungua hadi asilimia 2.6 ya Pato la Taifa kwa mwaka 2024/2025 kutoka asilimia 3.7 mwaka 2023/2024 kwa Tanzania Bara.
Bw.Tutuba ambaye pia ni Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania ameyasema hayo Julai 3,2025 makao makuu ndogo ya BoT jijini Dar es Salaam wakati akitangaza Riba ya Benki Kuu (CBR) kwa robo ya tatu ya mwaka 2025 ambayo ni asilimia 5.75.

Riba hiyo imeshuka kutoka asilimia 6 ambayo ilidumu kwa robo mbili mfululizo na itadumu kuanzia Julai hadi Septemba, mwaka huu kabla ya Oktoba kutangazwa riba nyingine.

Uamuzi wa kushusha riba hiyo ni utekelezaji wa sera ya fedha ili kuhakikisha riba ya mikopo ya siku saba baina ya benki inabaki ndani ya wigo wa asilimia 3.75 hadi 7.75.

Katika mkutano huo ambao uliwakutanisha pamoja viongozi wa benki na waandishi mbalimbali wa vyombo vya habari,Gavana Tutuba amesema, ukuaji huo wa uchumi umechagizwa na sekta za kilimo,huduma za fedha, bima, michezo, madini na ujenzi.

Akizungumzia kuhusu mikopo kwa sekta binafsi, Gavana Tutuba amefafanua kuwa, ilikuwa kwa wastani wa asilimia 16.7 katika robo ya pili ya mwaka 2025.

Pia,amesema mikopo chechefu ilipungua hadi asilimia 3.4 mwezi Mei,2025 ikiwa ni chini ya kiwango kinachohimilika cha asilimia 5.0.

Kwa upande wa mfumuko wa bei kwa Tanzania Bara, Gavana Tutuba amesema ulikuwa wastani wa asilimia 3.2 katika robo ya pili ya mwaka 2025, ukiakisi utekelezaji madhubuti wa sera ya fedha na utulivu wa bei za bidhaa zisizo za chakula na zile za nishati.

Mbali na hayo amesema kuwa, mfumuko wa bei za chakula uliongezeka kidogo, kutokana na changamoto za usafirishaji zilizosababishwa na mvua kubwa katika baadhi ya maeneo nchini.

Akizungumzia kwa upande wa Zanzibar,Gavana Tutuba amesema mfumuko wa bei ulipungua hadi asilimia 4.2 mwezi Mei 2025, kutoka asilimia 5.3 Mei mwaka jana, hali iliyochangiwa zaidi na kushuka kwa bei za chakula visiwani humo.

Kwa upande wa thamani ya shillingi dhidi ya dola ya Marekani, Gavana Tutuba amesema ilishuka kwa kasi ndogo ya asilimia 0.2 kwa mwaka ulioishia Juni,2025 ikilinganishwa na kushuka kwa asilimia 12.5 katika katika kipindi kama hicho mwaka jana.

Gavana Tutuba amesema, utulivu huo umechangiwa na kuongezeka kwa ukwasi wa fedha za kigeni kutokana na mapato ya utalii,mauzo ya bidhaa nje ya nchi ikiwemo tumbaku na dhahabu.

Amesema, utekelezaji madhubuti wa sera ya fedha na usimamizi wa kanuni zinazotaka miamala ya fedha ya ndani ya nchi kufanyika kwa shilingi vimechangia kwa kiasi kikubwa katika kuimarisha utulivu wa shillingi ya Tanzania.

Gavana Tutuba amefafanua kuwa, ongezeko la ununuzi wa dhahabu kutoka ndani ya nchi kwa ajili ya kuongeza akiba ya fedha za kigeni lilichangia kuongeza imani kwa sarafu ya Tanzania.

Amesema, tangu Benki Kuu ianze kununua dhahabu iliyosafishwa Oktoba 1, mwaka jana hadi Juni 30, mwaka huu wamenunua tani 6.6 za dhahabu hiyo yenye thamani ya Dola za Marekani milioni 718 ambapo mwaka huu wataendelea kununua.

Kuhusu akiba ya fedha za kigeni,Gavana Tutuba amesema,imefikia zaidi ya dola bilioni 6 ikiwa ni kiwango cha juu katika kipindi cha hivi karibuni.

Amesema, kwa upande wa Zanzibar inakadiriwa kuwa na ziada ya dola milioni 611.1 mwaka 2024/2025 kutoka ziada ya dola milioni 428.5 mwaka uliopita.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news