DAR-Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Cosato Chumi (Mb.), amekutana na kuzungumza na Balozi wa Taifa la Qatar, Mhe. Fahad Rashid Al Marekhi, katika Ofisi Ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam.
Viongozi hao wamejadiliana namna ya kuendelea kushirikiana ili kuimarisha ushirikiano kiuchumi na kijamii kwa maslahi ya Mataifa hayo.
Mhe. Naibu Waziri amelipongeza Taifa la Qatar kwa kuendelea kushiriki katika utatuzi wa migogoro duniani.
Tanzania na Qatar zimekuwa zikishirikiana kwa karibu kwa muda mrefu katika sekta za uwekezaji, biashara, elimu, afya, maji na utalii.
Kwa upande wake Mhe. Balozi Fahad Rashid Al Marekhi ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa kuendeleza ushirikiano wa maslahi ya pande zote kati ya Taifa lake Qatar na Tanzania.
Tanzania na Qatar zilianzisha ushirikiano wa kidiplomasia na baadae kufungua Ofisi za Ubalozi jijini Dar es Salaam mwaka 2012 na jijini Doha mwaka 2015 uhusiano ambao umeendelea kuimarika siku hadi siku.












