Ofisi ya Msajili wa Hazina yalenga kukusanya shilingi trilioni 2

PWANI-Ofisi ya Msajili wa Hazina (OMH) imejiwekea lengo la kukusanya kiasi cha shilingi trilioni 2 kama mapato yasiyo ya kikodi katika mwaka wa fedha 2025/26.
Hayo yamesemwa Julai 28, 2025 na Msajili wa Hazina,Bw.Nehemiah Mchechu wakati wa ufunguzi wa mafunzo elekezi ya siku nne kwa wakuu wa taasisi za umma yaliyoandaliwa na OMH kwa kushirikiana na Taasisi ya Uongozi.

Kiasi kinachotarajiwa kukusanywa ni zaidi ya lengo la shilingi trilioni 1.6 ambalo Serikali iliiwekea Ofisi ya Msajili wa Hazina kukusanya mwaka huu wa fedha.
“Ili tuweze kufikia lengo letu la kukusanya shilingi trilioni 2 itatubidi tuongeze bidii kwa asilimia 100 ya tulivyokuwa tunafanya mwaka wa fedha uliopita,” alisema Bw. Mchechu.

Katika mwaka wa fedha uliopita (2024/25) Ofisi ya Msajili wa Hazina ilikusanya kiasi cha shilingi trilioni 1.028 kama mapato yasiyo ya kikodi.

Miongoni mwa vyanzo vikuu vya mapato yasiyo ya kikodi ni Gawio ambapo mapato haya yanatokana na Mashirika na Taasisi zinazofanya biashara na yanakusanywa kwa mujibu wa Sheria ya Makampuni SURA 212 (Kifungu cha 180) na Sheria ya Mashirika ya Umma Sura 257 (Kifungu cha 15(2)(b)).
Vyanzo vingine ni michango ya asilimia 15 ya mapato ghafi ambapo Kifungu cha 12 (3) cha Sheria ya Fedha za Umma Sura 348 kinazitaka taasisi za umma (zisizo kwenye kundi la gawio) kuwasilisha asilimia kumi na tano ya mapato ghafi kwenda Mfuko Mkuu wa Serikali.

Pia,kuna mapato mengineyo ambayo huhusisha asilimia 70 ya mapato ya ziada ya taasisi za umma, marejesho ya mikopo na riba na mawasilisho yatokanayo na mtambo wa kuhakiki na kuwezesha mawasiliano (TTMS) kati ya Tanzania na nchi nyingine.
Msajili wa Hazina anaamini kuwa,mafunzo elekezi kwa kundi hili la pili linalojumuisha watendaji wakuu 114 wakiwemo walioteuliwa hivi karibuni pamoja na walioko katika nafasi zao kwa muda mrefu,lakini hawakubahatika kupatiwa mafunzo, yatakuwa chachu ya mageuzi katika mashirika ya umma.

Lengo la mafunzo haya ni kuwaimarisha wakuu wa taasisi katika nyanja za uongozi na maadili, uwajibikaji wa kifedha na usimamizi wa uwekezaji wa umma ambao hadi kufikia mwaka 2023/24 umefikia takribani Sh86.25 trilioni, ambapo kiasi hiki kimewekezwa katika taasisi za umma 252 na kampuni ambazo Serikali ina hisa chache 56.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news