Rais Dkt.Mwinyi aishukuru Canada

ZANZIBAR-Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi ameishukuru Serikali ya Canada kwa kuendeleza ushirikiano wa kidiplomasia na misaada ya maendeleo kwa Tanzania, ikiwemo Zanzibar, hususan katika sekta mbalimbali za kijamii na kiuchumi.
Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo alipokutana na Balozi wa Canada nchini Tanzania, Mhe. Emily Burns, aliyefika Ikulu Zanzibar leo, tarehe 10 Julai 2025.

Rais Dkt. Mwinyi amesema kuwa Tanzania inathamini ushirikiano wa muda mrefu uliopo kati ya nchi hizo mbili, ushirikiano ambao umekuwa nyenzo muhimu katika kuimarisha uhusiano wenye mafanikio na manufaa kwa pande zote mbili.
Rais Dkt. Mwinyi amemweleza Balozi huyo kuwa bado kuna fursa nyingi zaidi za ushirikiano, akizitaja sekta za uchumi wa buluu, uvuvi wa bahari kuu, mafuta na gesi, kilimo cha mwani na biashara kama maeneo muhimu ya uwekezaji.

Amefafanua kuwa,Zanzibar inategemea sekta ya utalii kama sekta ya kipaumbele inayochangia asilimia 30 ya pato la taifa, na kuiomba Canada kuhamasisha wawekezaji kuwekeza zaidi katika sekta hiyo pamoja na sekta ya biashara kwa ujumla.
Rais Dkt. Mwinyi pia ametoa wito wa kuanzishwa kwa jukwaa la pamoja kati ya wafanyabiashara wa Canada na Zanzibar, ili kutambua fursa mpya za kiuchumi na uwekezaji, huku akiwaalika wawekezaji wa sekta binafsi kuwekeza Zanzibar.

Akizungumzia Uchaguzi Mkuu ujao, Rais Dkt. Mwinyi ameihakikishia Canada kuwa uchaguzi huo utakuwa huru, wa amani na utulivu, kufuatia juhudi za Serikali kuendeleza mafanikio ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa na kuimarisha maridhiano kati ya vyama vya siasa.
Kwa upande wake, Balozi Emily Burns amepongeza maendeleo yanayofikiwa Zanzibar, hasa katika sekta ya uchumi wa buluu na utalii.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news