DODOMA-Miongoni mwa Mashujaa waliopigana vita ya Kagera, Brigedia Jenerali mstaafu na Balozi Francis Mndolwa amewaasa waandishi wa habari nchini kuandika habari zenye kuijenga jamii, kuleta heshima kwa Taifa, na kukuza uzalendo ikiwa ni sehemu ya ujenzi juhudi za mashujaa hao pamoja na waasisi wa Taifa la Tanzania.
Mmoja wa Mashujaa aliyeshiriki katika Vita ya Kagera, Brigedia Jenerali Mstaafu Balozi Francis Mndolwa akielekea kwenye eneo la Mnara wa Mashujaa kuweka Shoka kama ishara ya kuwaenzi Mashujaa wa Kitanzania waliotangulia mbele za haki.
Akizungumza na waandishi wa habari katika katika maadhimisho ya kumbukumbu ya Mashujaa nchini , Balozi Mndolwa aliwataka kuenzi kazi yao kama sehemu ya mchango mkubwa kwa Taifa.
"Waandishi muandike habari ambazo zitawainua na kuwaheshimisha. Waandishi wote wa habari mnapaswa kuwa wazalendo,nchi hii imetoka mbali, inahitaji msaada wa kila mmoja wenu ili tuendelee kuwa na amani.”
Burudani ikiendelea kutoka Kikundi cha Makutupora wakati wa sherehe za Maadhimisho ya Kumbukumbu ya Siku ya Mashujaa Tanzania zilizofanyika tarehe 25 Julai, 2025 katika Viwanja vya Mashujaa vilivyopo Mji wa Serikali Mtumba mkoani Dodoma.
Balozi Mndolwa aliwakumbusha waandishi kuhusu historia ya taifa, akitaja jinsi viongozi waasisi kama Mwalimu Julius Nyerere na Mzee Abeid Amani Karume walivyoweka msingi wa mshikamano wa kitaifa, amani na maendeleo.
Alisisitiza kuwa, Tanzania imeweza kudumisha utulivu wa muda mrefu licha ya changamoto zinazozikumba nchi nyingi jirani.
Mnara wa Mashujaa.
"Nchi nyingi zinazotuzunguka zimebomoka, zimepata matatizo, lakini tuwashukuru taasisi zetu, Mwalimu Nyerere, Mzee Karume, kwa kuwaandaa wananchi ambao sasa wanaendelea na juhudi zao na nchi kuwa na amani,” amesema.
Mndolwa pia alitoa wito kwa waandishi na Watanzania kwa ujumla kujiepusha na kuiga migogoro ya mataifa makubwa duniani.
Vikosi vya Ulinzi na Usalama vikifanya Gwaride maalum lililoandaliwa wakati wa sherehe za Maadhimisho ya Kumbukumbu ya Siku ya Mashujaa nchini tarehe 25 Julai, 2025.
"Msiwe na mwendo wa upinzani wa dunia, tunawaona Warusi, Wachina wakigombana na Marekani ,huo ni ugomvi wao wa dunia, hatuutaki. Tunataka hivi tulivyo, lazima tushirikiane,” aliongeza kwa msisitizo.
Maadhimisho ya Siku ya Mashujaa ni wakati wa kukumbuka na kuthamini mchango wa watetezi wa taifa waliopigania uhuru, usalama, na heshima ya nchi.




