ZANZIBAR-Viongozi wa Taasisi ya Sayansi na Teknolojia Karume (KIST) wametakiwa kuanzisha Dawati la Jinsia ili kutii agizo la viongozi wakuu wa Serikali.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsi, Wazee na Watoto ,Abeidah Abdalla Rashid ameyasema hayo wakati wa ziara ya kuhamashisha, kuanzishwa kwa Dawati la Kijinsia huko Bweni Wilaya ya Magharibi B.
Amesema,viongozi wakuu wa Serikali wametoa miongozo wa kuanzishwa madawati ya kijinsia vyuo vikuu na kati ili kupiga vita vitendo viovu nchini.
Amesema,Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi yupo mstari wa mbele katika kupiga vita vitendo vya udhalilishaji, hivyo kuanzisha kwa dawati hilo ni kuunga mkono juhudi za kiongozi huyo.
Mbali na hayo,Katibu Abeidah ameomba kuweka chumba maalum ili kusaidia Waalimu na wanafunzi kunyonyesha Watoto wao kwa lengo la kuondosha usumbufu unaoweza kukitokeza.
Naye Mkurugenzi Idara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia na Watoto,Siti Abasi Ali amesema kuanzishwa kwa dawati hilo, kutawawezesha walimu,wanafunzi na watoa huduma kupeleka changamoto zao na kupatiwa ufumbuzi wa haraka.

Hata hivyo, amesema Serikali kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto inaahidi kutoa mafunzo na fursa mbalimbali zinazoweza kupatikana ili Dawati hilo liweze kuimarika.
Kwa upande wake Mkuu wa Taasisi ya Sayansi na Teknolojia Karume (KIST), Dkt.Mahmoud Alawi amesema,ujio wa viongozi hao, kumewapa faraja na kuwa chachu ya maendeleo na kuomba kupatiwa mafunzo ya mara kwa mara ili dawati hilo liweze kufanya kazi kwa ufanisi.