DODOMA-Serikali imesema kuwa, marekebisho ya sheria yaliyofanyika hivi karibuni yameongeza nguvu zaidi kwa kutambua makosa ya rushwa yanayofanyika katika maeneo mbalimbali ikiwemo upande wa burudani, michezo,chaguzi na mengineyo.
.jpeg)
Hayo yamebainishwa leo Julai 11,2025 jijini Dodoma na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mheshimiwa George Simbachawene wakati akifungua Kongamano la Maadhimisho ya Siku ya Mapambano Dhidi ya Rushwa barani Afrika.
Kaulimbiu ya maadhimisho ya mwaka huu ni kukuza na kulinda heshima ya binadamu katika mapambano dhidi ya rushwa.
Amesema, kupitia Sheria ya Kupambana na Rushwa Na. 11 ya mwaka 2007, Taasisi ya Kuzuia na Kupambaba na Rushwa Tanzania (TAKUKURU) imepewa mamlaka ya kuhakikisha kuwa rushwa inatokomezwa nchini.
Vilevile amesema,Serikali imeendelea kuipatia TAKUKURU rasilimali fedha, kibali cha kuajiri watumishi wapya na vitendea kazi na samani za ofisi ili kuongeza ufanisi wake wa kazi.
Pia, Waziri Simbachawene ametoa wito kwa wadau wote kuja na mbinu mpya ambazo hazijazoeleka ili kusaidia kuboresha mapambano dhidi ya rushwa.
"Kwa hiyo tunapaswa kuangalia namna taasisi zetu zinavyohudumia wananchi, kwani huduma bora na haki ni kipimo muhimu cha mafanikio yetu."
Aidha,Mheshimiwa Simbachawene amesema, Mkataba wa Umoja wa Afrika wa Kupambana na Rushwa umeweka misingi ya nchi wanachama kushirikiana katika mafunzo, sheria na mikakati ya kuzuia na kupambana na rushwa kwa pamoja.
Waziri Simbachawene amesema, kupitia mkataba huo, nchi zimewekewa wajibu wa kushughulikia kwa haraka maombi ya vyombo vya dola vinavyohusika na upelelezi, mashitaka, na utoaji wa adhabu kwa watuhumiwa wa makosa ya rushwa na yale yanayohusiana nayo.
Naye Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Profesa Palamagamba Kabudi, amesema,vitendo rushwa katika jamii havipaswi kufumbiwa macho.
Profesa Kabudi amefafanua kuwa,rushwa inapozidi katika jamii huwa inadhoofisha huduma mbalimbali, hivyo hukosesha watu haki,usawa na kuvuruga utu wa kibinadamu.
Kutokana na changamoto hiyo ambayo rushwa inawapa furaha wachache,amesema kila mmoja wetu anapaswa kushirki kikamilifu katika mapambano dhidi ya vitendo vya rushwa.Kwa kina tazama video hapa chini;