Tanzania,IFRC wajadili kuimarisha ushirikiano katika masuala ya kibinadamu Afrika Mashariki

DODOMA-Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki, Mhe. Denis Londo (Mb) amelishukuru Shirikisho la Kimataifa la Vyama vya Msalaba Mwekundu na Hilali Nyekundu (IFRC) kwa mchango wake mkubwa katika kusaidia jamii za Kitanzania, hasa wakati wa majanga na dharura.

Pia, amesisitiza umuhimu wa kushirikiana kwa karibu na taasisi za ndani kama Chama cha Msalaba Mwekundu Tanzania na Wizara husika ili kuhakikisha huduma zinafika kwa wakati na kwa ufanisi.
Mhe. Londo alitoa shukrani hizo alipokutana na ujumbe wa IFRC) jijini Dodoma Julai 16, 2025.

Ujumbe huo uliokuwa ukiongozwa na Bw. Mohamed Babiker, Kiongozi Mkuu wa IFRC kwa Ukanda wa Afrika Mashariki mwenye makazi yake Juba, Sudan Kusini ulifika Wizarani ukiambatana na Katibu Mkuu wa Chama cha Msalaba Mwekundu Tanzania, Bi. Lucy Pande.
Mazungumzo hayo yalijikita zaidi kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania na IFRC katika masuala ya kibinadamu na maendeleo ya kikanda, hususan katika nchi za Tanzania, Uganda na Sudan Kusini.

Bw. Babiker alielezea dhamira ya dhati ya IFRC ya kuendeleza ushirikiano na Tanzania katika kujenga uwezo wa jamii kukabiliana na majanga, kulinda maisha ya watu walioko kwenye mazingira hatarishi, na kuendeleza misingi ya huduma za kibinadamu kama usawa, utu na kutoa huduma bila upendeleo.
Aidha, alihimiza umuhimu wa Tanzania kushiriki katika mikutano mikuu ya kimataifa ya IFRC inayofanyika kila baada ya miaka minne ambapo maamuzi mbalimbali yanafanyika kama utungaji na upitishaji wa sera na mwelekeo wa kimataifa wa masuala ya kibinadamu.

Aliongeza kuwa,Tanzania inaweza kuwa kitovu cha kikanda cha mafunzo, kutokana na mazingira yake ya usalama na utulivu.
Vilevile, Bw. Babiker alieleza kuwa IFRC imeanzisha warsha maalum kwa wanawake viongozi kutoka nchi mbalimbali za Afrika, ambapo wanawake kutoka Tanzania na nchi jirani wamealikwa kushiriki kama sehemu ya kuimarisha uongozi wa wanawake katika masuala ya kibinadamu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news