Vyama vya ushirika vina mchango mkubwa katika kukuza uchumi-Mheshimiwa Abdulla

ZANZIBAR-Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdulla amesema, vyama vya ushirika vina mchango mkubwa katika kukuza uchumi, kuimarisha mshikamano wa kijamii na kuweka usawa wa kiuchumi kwa wananchi.
Akizungumza katika maadhimisho ya Siku ya Ushirika Duniani yaliyofanyika Kizimkazi, Mkoa wa Kusini Unguja, ambapo alimuwakilisha Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, Mhe. Hemed amesema vyama vya ushirika vimejikita zaidi katika shughuli za kiuchumi na vinapaswa kuthaminiwa kwa mchango wake mkubwa katika maendeleo ya taifa.

Amesema ipo haja ya kufanya mageuzi makubwa katika sekta ya ushirika Zanzibar ili kuviwezesha vyama hivyo kuendana na wakati na kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao.

Ameeleza kuwa tayari serikali imefanikiwa kuviunganisha vyama 383 vya uzalishaji katika vyama vya Akiba na Mikopo (SACCOS) Unguja na Pemba, hatua iliyowapa wanachama uwezo wa kupata mitaji kwa ajili ya shughuli za maendeleo.

Mhe. Hemed ameipongeza Ofisi ya Rais, Kazi, Uchumi na Uwekezaji kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi katika kufanya utafiti wa kina kuhusu sekta ya ushirika, ambao umebaini changamoto kadhaa zikiwemo mifumo ya usajili, usimamizi, uendeshaji na ukosefu wa takwimu sahihi.

Amesema serikali imejipanga kupitia upya sheria ya vyama vya ushirika namba 15 ya mwaka 2018, sera ya maendeleo ya ushirika ya mwaka 2014 pamoja na kanuni zake za mwaka 2019, ili kuweka mfumo imara unaokidhi mahitaji ya sasa.

Pia, serikali inapanga kuanzisha mfumo wa kidijitali wa usajili, ufuatiliaji na usimamizi wa vyama vya ushirika pamoja na taasisi ya ukaguzi wa hesabu kwa ajili ya kuongeza uwajibikaji na ufanisi.

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Kazi, Uchumi na Uwekezaji Zanzibar, Mhe. Shariff Ali Shariff amesema zaidi ya vyama 7,000 vya ushirika vimesajiliwa Zanzibar, kwa lengo la kushirikiana katika shughuli za kiuchumi, huku akibainisha kuwa serikali itaendelea kushirikiana na wadau wote kuimarisha sekta hiyo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news