NA GODFREY NNKO
MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imewakamata watuhumiwa sita wakiwemo raia wawili wa China ambao wamefahamika kwa majina ya Chein Bai na Qixian Xin eneo la Posta jijini Dar es Salaam wakisafirisha dawa za kulevya.
Dawa hizo zina uwezo wa kufuta kumbukumbu zote kichwani kwa mtumiaji, hivyo kuchochea kufanyiwa vitendo vya kikatili hususani maeneo ya starehe na hata kusababisha kifo cha ghafla.
Hayo yamesemwa Julai 9,2025 jijini Dar es Salaam na Kamisha Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake.
Kamishna Jenerali Lyimo amesema,dawa za kulevya walizokamatwa nazo ni aina ya Methamphetamine gramu 1.42, dawa tiba zenye asili ya kulevya aina ya frunitrazepam (rohypnol) vidonge 1,000 na Ketamine zenye uzito wa kilogramu 1.92.
“Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama tulifanya operesheni ambapo tumefanikiwa kuwakamata watuhumiwa sita wakiwemo raia wawili wa China wakiwa na dawa za kulevya eneo la Posta jijini Dar es Salaam.
"Dawa hizo walikuwa wameweka katika vitu ambavyo unaweza kudhani ni kitabu kumbe sio ila ndani yake wameweka dawa hizo.Tunatoa rai kwa wageni wanaokuja nchini kwetu wahakikishe wanafanya shughuli halali ambazo wamekuja kuzifanya badala ya kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya.
“Tutaendelea na operesheni na yeyote ambaye anajihusisha na biashara hii tutamtia hatiani.Hivyo nisisiteze wageni mlioko nchini fanyeni kazi halali zilizowaleta,"amefafanua Kamishna Jenerali Lyimo.
Tags
Breaking News
DCEA
DCEA Tanzania
Habari
Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA)

