DAR-Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Bw. Ngosha Magonya na Bi. Esther Manyesha, wametembelea banda la BoT katika Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Sabasaba yanayoendelea katika viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam.
Katika ziara hiyo, wajumbe hao wamejionea kwa karibu jinsi Benki Kuu inavyotoa elimu kwa umma kuhusu majukumu yake mbalimbali, yakiwemo utekelezaji wa sera ya fedha, kudhibiti mfumuko wa bei, na mchango wake katika kuimarisha uchumi wa taifa.Aidha, wamepata maelezo kuhusu fursa za uwekezaji kupitia dhamana za serikali za muda mfupi na muda mrefu.
Elimu nyingine inayotolewa ni kuhusu mifumo ya malipo ya taifa ambayo inawezesha miamala kufanyika kwa haraka, salama na kwa ufanisi zaidi.
Vilevile, wananchi wanaelezwa kuhusu namna Benki Kuu inavyosimamia taasisi za fedha nchini ili kuhakikisha zinatoa huduma kwa ufanisi, kwa uwazi, na kwa kuzingatia sheria na kanuni za sekta ya fedha.
Katika banda hilo, wananchi pia wanapata taarifa kuhusu utaratibu wa kushughulikia malalamiko ya watumiaji wa huduma za kifedha, pamoja na taratibu za ajira na utumishi ndani ya Benki Kuu.
Vilevile, wamepatiwa maelezo kuhusu programu za mafunzo zinazotolewa na Chuo cha BoT kwa lengo la kujenga uwezo wa wataalamu wa masuala ya fedha na kibenki.
Aidha, BoT inatoa elimu maalum kuhusu namna ya kutambua alama za usalama katika noti za Tanzania, pamoja na mbinu sahihi za kuzitunza noti na sarafu ili kuhakikisha ubora wa fedha zetu unaendelea kudumishwa.
Sambamba na hayo, wamehimiza umuhimu wa kuendeleza juhudi za kufikia makundi mbalimbali ya jamii kupitia elimu ya fedha, ikiwa ni pamoja na vijana, wajasiriamali, na wananchi wa kawaida, ili kukuza maarifa na mchango wao katika ustawi wa uchumi wa taifa.








