KILIMANJARO-Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba ameshiriki Maadhimisho ya Miaka Mitatu ya kuanzishwa kwa Kituo cha Michezo kwa Vijana kilichopo Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro cha Kilimanjaro Wonder's Sports Centre (KWSC).
Akiwa mgeni rasmi katika maadhimisho hayo yaliyofanyika katika Viwanja vya Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi (Moshi Co-operative University, MoCu) amewapongeza waandaaji na maadhaminisho kwa namna ambavyo wanaunga mkono jitihada za Serikali katika kuibua na kukuza vipaji vya michezo nchini.
Mheshimiwa Dkt.Nchemba amesema, Serikali imeendelea kuweka mazingira rafiki katika kuhakikisha inakuza na kulea vipaji vya wanamichezo ndani na nje ya nchi ili kuwa na vijana wenye uwezo katika soka na kuwasaidia kukua kiuchumi.
"Hongereni sana wadau wa KWSC kwa ushirikiano na Kili Icon kwa maandalizi haya yenye nia ya kuibua na kukuza vipaji vya wanamichezo nchini, mnaiunga mkono Serikali katika jambo hili kuhimu kwenye nyanja ya michezo,"lisema Dkt. Nchemba.
Maadhimisho hayo yamehudhuriwa na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Mhe. Nurdin Babu, Mkuu wa Wilaya ya Moshi Mhe. Godfrey Mnzava, Mkurugenzi wa Kituo cha KWSC ndugu Lauren Kinabo na Viongozi mbalimbali wa Serikali, baadhi ya Wachezaji kutoka Timu zinazoshiriki Ligi Kuu nchini na nje ya nchi, Wanafunzi na Wananchi wa Mkoa huo.





