Waziri Kombo ashirirki kikao cha 47 cha Baraza la Mawaziri AU

MALABO-Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb.) ameshiriki katika kikao cha 47 cha Baraza la Mawaziri wa Umoja wa Afrika (AU) kinachoendelea jijini Malabo, Equatorial Guinea.
Baraza hilo limejadili Ripoti ya Kamati ya Wawakilishi wa Kudumu wa AU (Permanent Representative’s Committee - PRC) ambapo Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imechangia hoja mbalimbali za muhimu ikiwemo kuunga mkono kuidhinishwa kwa mapendekezo ya bajeti ya Umoja wa Afrika kwa mwaka 2026 ambayo imezingatia hali halisi ya uchumi wa nchi wanachama.
Pia, Tanzania imesisitiza umuhimu wa Kamisheni kukamilisha Mpango Mkakati wa Miaka Mitano ili kuhakikisha mipango ya mwaka mmoja mmoja inaendana na vipaumbele vya Mpango wa Pili wa Miaka Kumi ya Utekelezaji wa Agenda 2063.

Aidha, Tanzania imetoa rai na ushauri kwa AU kutumia vyema fursa ya Jamhuri ya Afrika Kusini kuwa mwenyeji wa mkutano wa G20, 2025 kupenyeza vipaumbele vya Bara la Afrika hasa kwenye maeneo ya upatikanaji sawa wa ufadhili wa maendeleo, mageuzi kwa taasisi za fedha za kimataifa, na ufumbuzi wa haraka wa udhaifu unaoongezeka wa madeni barani Afrika, kupata ufadhili wa muda mrefu wa miundombinu, na kukabiliana na hali ya hewa, na mseto wa kiuchumi.
Mkutano huu wa 47 wa Baraza la Mawaziri unautangulia Mkutano wa Saba wa Kamati ya Uratibu ya Umoja wa Afrika utakaohudhuriwa na Wakuu wa Nchi na Serikali wa Kamati ya Uongozi ya Umoja wa Afrika (AU Bureau of Assembly), na Wenyeviti wa Jumuiya 8 za Kikanda Julai 13, 2025.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news