ZANZIBAR-Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Zanzibar, Mheshimiwa Fatma Hamad Rajab, amelipongeza Baraza la Kiswahili Zanzibar (BAKIZA) kwa jitihada kubwa wanazozichukua katika kuisimamia na kuifundisha lugha ya Kiswahili.
Akizungumza katika Skuli ya Dr. Samia Suluhu Hassan, Mwanakwerekwe, wakati akifungua mafunzo ya siku moja ya uandishi wa insha kwa wanafunzi waliofanya vizuri katika mashindano ya uandishi wa insha, Katibu Mkuu alisema lugha ya Kiswahili ni urithi wa Taifa unaopaswa kulindwa na kuendelezwa.
“Tuna kila sababu na sifa ya kujivunia katika kukizungumza Kiswahili chetu. Tuifanyie haki lugha yetu,” alisisitiza Mhe. Fatma.
Aidha, aliwapongeza walimu kwa kazi kubwa wanayoifanya katika kuwafundisha wanafunzi kutumia lugha ya Kiswahili kwa ufasaha, huku akiwataka wanafunzi hao kuwa makini na kuwasikiliza walimu wao ili kuongeza umahiri wao katika lugha hiyo.
Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa Baraza la Kiswahili Zanzibar (BAKIZA), Dk. Mwanahija Ali Juma, alisema kuwa uandishi wa insha unawasaidia wanafunzi kupata maarifa mapana yatakayowasaidia katika maisha yao ya kitaaluma na kijamii.
“Uandishi wa insha una umuhimu mkubwa kwani unawafanya wanafunzi kutambua matumizi ya lugha sanifu, vituo vya alama na msamiati sahihi,” alifafanua Dk. Mwanahija.
Hata hivyo, alieleza kuwa bado kuna changamoto kwa baadhi ya wanafunzi kushindwa kutumia lugha sanifu, kukosa ubunifu pamoja na kutozingatia matumizi ya msamiati, jambo linaloharibu ladha ya Kiswahili fasaha.
Nao wanafunzi walioshiriki mafunzo hayo walisema kuwa yamewapa mbinu mpya zitakazowasaidia kufanya vizuri katika mashindano yajayo pamoja na kuimarisha uwezo wao wa kujibu mitihani.
