DAR-Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Dkt.Yamungu Kayandabila amesema, kuwa Benki Kuu inaendelea kusimamia uthabiti wa sekta ya fedha ili kuchochea ukuaji endelevu wa uchumi na maendeleo ya taifa kwa ujumla.
Dkt.Kayandabila ameyasema hayo leo Agosti 27,2025 aliposhiriki katika mjadala wa Jukwaa la Biashara la Maafisa Watendaji Wakuu, lililofanyika jijini Dar es Salaam.
Amesema kuwa, sekta ya fedha nchini inaendelea kukua na kuimarika, hivyo ni lazima iwe ya ushindani, jumuishi, yenye ufanisi na gharama nafuu.
Aidha, amebainisha kuwa Benki Kuu imeendelea kuweka mazingira rafiki kwa sekta mbalimbali nchini, ikiwemo kilimo, ambapo shilingi trilioni moja imetengwa kwa ajili ya kusaidia mikopo ya kilimo. Kupitia Mfuko huo, benki zinazoshiriki zinatoa mikopo kwa riba isiyozidi asilimia 10.
Aliongeza kuwa, BoT inaendelea kufanya mapitio ya mfuko huo ili kusaidia upatikanaji wa mikopo kwa sekta nyingine muhimu kama vile uzalishaji na nishati.


