MBEYA-Benki Kuu ya Tanzania (BoT) tawi la Mbeya limeibuka mshindi wa kwanza wa jumla katika Maonesho ya Nanenane kwa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini. Maonesho hayo yamefanyika kuanzia tarehe 1 hadi 8 Agosti 2025 katika Uwanja wa John Mwakangale jijini Mbeya.
Ushindi huo unathibitisha jitihada za Benki Kuu katika kutoa elimu kwa wananchi, ili kuwajengea uelewa kuhusu masuala ya fedha na kuhimiza matumizi ya taasisi rasmi za fedha kwa lengo la kunufaika na huduma kama vile uwekaji akiba, uwekezaji na mikopo.
Aidha, utoaji wa elimu hii unawezesha kujenga uaminifu kati ya wananchi na sekta ya fedha, sambamba na kuwapa maarifa ya kutambua na kutumia fursa mbalimbali zilizopo katika uchumi wa nchi. Hatua hii inachangia katika kujenga jamii yenye maarifa ya kifedha na yenye uwezo wa kushiriki ipasavyo katika maendeleo ya Taifa.

