KUALA LUMPUR-Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Bw. Emmanuel Mpawe Tutuba amekutana na kufanya majadiliano na wawekezaji na wafanyabiashara mbalimbali nchini Malaysia kwa lengo la kuwahamasisha kuwekeza nchini Tanzania katika sekta mbalimbali.
Amesisitiza kuwa, Tanzania ina mazingira bora na rafiki kwa uwekezaji kutokana na hali ya amani na utulivu wa kisiasa, pamoja na sera madhubuti na wazi kwa wawekezaji wanaokidhi vigezo na masharti ya kisheria.Amebainisha kuwa, Serikali ya Tanzania iko tayari kutoa ushirikiano wa kutosha kwa wawekezaji hao ili kuwawezesha kuendesha shughuli zao kwa mafanikio.
Gavana Tutuba ameeleza kuwa, Tanzania ina nguvu kazi ya kutosha pamoja na miundombinu ya msingi inayowezesha uwekezaji, ikiwemo barabara, reli, umeme na maji.
Aidha, amesisitiza kuwa, Tanzania ina fursa nyingi kutokana na jiografia yake ya kipekee ikiwa imezungukwa na bahari, mito, maziwa na milima ya kuvutia, na ni nchi inayofikika kwa urahisi.
Pia, Gavana Tutuba ametoa wito kwa wawekezaji hao kuangazia sekta kama vile utalii, afya, nishati, madini, kilimo, misitu, huduma za kifedha na sekta nyingine zenye mchango mkubwa kwa maendeleo ya uchumi wa Taifa.
Kwa upande wao, wawekezaji kutoka Malaysia wakiongozwa na Prof. Chris Tan wamemshukuru Gavana Tutuba na ujumbe wake kwa kutembelea Malaysia na kutenga muda kufanya mazungumzo nao.
Pia, wameeleza kuwa, wapo tayari kuanzisha ubia na kutumia fursa zilizopo kutokana na uhusiano mzuri baina ya Malaysia na Tanzania.
Katika hatua nyingine, Gavana Tutuba na ujumbe wake walitembelea Ofisi za Ubalozi wa Tanzania nchini Malaysia na kufanya mazungumzo na wafanyakazi wa ubalozi huo wakiongozwa na Kaimu Balozi, Mhe. Zainab Mrutu.
Katika mazungumzo hayo, Gavana Tutuba aliwataka watumishi wa ubalozi huo kuendelea kuiwakilisha nchi kwa weledi na kuhamasisha uwekezaji kwa kueleza kwa kina fursa mbalimbali za kiuchumi zilizopo Tanzania.
Aidha, aliwasisitiza kuendelea kutangaza vivutio mbalimbali vya utalii vilivyopo nchini ili kuongeza idadi ya watalii wanaotembelea Tanzania, kuongeza mapato ya fedha za kigeni na kuchangia ukuaji wa uchumi wa Taifa.


