NA GODFREY NNKO
WAANDISHI wa habari nchini Tanzania wametakiwa kuendelea kuzingatia misingi, maadili na miiko ya uandishi wa habari hususani kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29,2025 ili kupitia kalamu, majukwaa na vyombo vyao vya habari waweze kutoa taarifa sahihi kwa ustawi wa jamii na Taifa kwa ujumla.


Wito huo umetolewa leo Agosti 14,2025 jijini Dar es Salaam katika mafunzo ya siku moja ya Uandishi wa Habari za Uchaguzi ambayo yameandaliwa na Kampuni ya Media Brains kwa kushirikiana na Taasisi ya Konrad Adenauer Stiftung (KAS).
Kupitia, mafunzo hayo wanahabari kutoka vyombo mbalimbali jijini Dar es Salaam wamejengewa uelewa wa kina kuhusu masuala mbalimbali ya uchaguzi ikiwemo sheria mpya ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi na Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani.
Awali, Mwakilishi Mkazi wa KAS nchini Tanzania, Peter Koch ameisitiza kuwa, waandishi wa habari wana jukumu muhimu la kutoa taarifa zisizoegemea upande wowote na kuwasilisha habari mbalimbali zitakazowanufaisha wananchi hasa kabla, wakati na baada ya uchaguzi.
Koch amesema, shirika hilo linatambua na kuthamini mchango mkubwa wa vyombo vya habari ambavyo ni nguzo muhimu katika kustawisha demokrasia.
"Vyombo vya habari ni miongoni mwa nguzo kuu, vikifanya kazi kama daraja kati ya wananchi na viongozi,kwa hiyo waandishi wa habari wanaaminika katika kuwaelimisha, kuwafahamisha wananchi na kuwawajibisha viongozi, na kushiriki kujenga jamii iliyo huru na yenye taarifa sahihi.”
Kwa mujibu wa Koch, katika mazingira ya sasa yenye mabadiliko ya haraka ya taarifa, jukumu hilo limekuwa na uzito zaidi. Ndiyo maana mafunzo kuhusu demokrasia na namna bora ya kuripoti kwa wanahabari ni ya lazima kwa ustawi wa jamii na kidemokrasia.
Naye Afisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Media Brains, Bw.Jesse Kwayu amesema, kila mwanahabari anapaswa kutumia kalamu yake ipasavyo ili kuwaelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa kushiriki kikamilifu katika Uchaguzi Mkuu na kuchagua viongozi sahihi.

Bw.Kwayu amesema, mafunzo haya ni mwendelezo wa mafunzo ambayo tayari yameshafanyika mikoa kadhaa nchini yakilenga kuwajengea uwezo wanahabari ili waweze kufanya kazi zao bila upendeleo au upotoshaji wa taarifa hasa kipindi hiki cha Uchaguzi Mkuu.
Amebainisha kuwa, mafunzo hayo yanasaidia kukuza uelewa kuhusu uwazi, uwajibikaji, na utawala wa sheria ambazo ni nguzo muhimu katika uendeshaji wa demokrasia.
"Wengi wetu tunachukulia uchaguzi poa,lakini ukweli ni kwamba, hatupo sahihi.Siasa ni kila kitu kwetu sisi, hivyo uchaguzi ni hatua ya kwenda kuzitekeleza hizo siasa zenyewe, na wanasiasa ndiyo wanabeba hatima ya kusimamia rasilimali zetu, hivyo hatupaswi kuuchukulia poa uchaguzi, tukaelimishe wananchi umuhimu wa kushiriki uchaguzi na kuchagua viongozi sahihi."
Bw.Kwayu amebainisha kuwa,demokrasia mara nyingi huwa dhaifu pale ambapo uandishi wa habari unakuwa wa kuchochea au wa upande mmoja.
Kwa hiyo,amesema mafunzo haya yatawasaidia waandishi kuepuka taarifa za kashfa, kuheshimu faragha,kuepuka lugha ya chuki na kushughulikia masuala nyeti bila kuibua migawanyiko.
Ameongeza kuwa, waandishi waliopata mafunzo ya kutosha wana uwezo wa kufafanua masuala tata ya kisiasa na kijamii, na kuyaelezea kwa njia rahisi na ya kuvutia kwa umma.
Hali hiyo, kwa upande mwingine, amesema huhamasisha ushiriki wa wananchi katika masuala ya kiraia, ikiwasukuma kupiga kura, kuhudhuria mikutano ya hadhara, na kuwawajibisha viongozi.
Mbali na hayo, Bw.Kwayu amewataka wanahabari kuhakikisha wanawake ambao wanagombea wanapewa nafasi sawa za kupasa sauti na kunadi ilani na sera zao kupitia majukwaa sawa ya habari kama ilivyo kwa wanaume.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mwenza wa Media Brains, Bw.Absalom Kibanda amewahimiza wanahabari kuzingatia misingi,miiko,maadili ya uandishi wa habari bila kusahau kufuata sheria na miongozo yote inayohusiana na uchaguzi katika kutekeleza majukumu yao.
"Na hatupaswi kuwa sehemu ya ushabiki nazi wa vyama vya siasa,tunapaswa kuzingatia maadili,miiko na kufuata sheria za uchaguzi."
Bw.Kibanda pia, amewashauri waandishi kutathmini hali ya kisiasa, migogoro ya kihistoria na masuala ya usalama katika maeneo wanayoripoti ili kuhakikisha wanakuwa salama kabla na baada ya kutekeleza majukumu yao.
