Mfuko wa SELF watoa mikopo ya shilingi bilioni 196.9 kwa wananchi wa kipato cha chini

NA GODFREY NNKO

MFUKO wa SELF (SELF Microfinance Fund) umefanikiwa kuongeza upatikanaji wa huduma za mikopo ya shilingi bilioni 196.9 kwa wananchi wa kipato cha chini katika kipindi cha kuanzia mwaka 2021 hadi kufikia Juni 30, 2025.

Aidha,kiwango cha mikopo chechefu kipo chini ya asilimia 10 huku mfuko ukijiendesha kwa kupata faida.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa SELF, Bi. Santieli Yona ameyasema hayo leo Agosti 15,2025 jijini Dar es Salaam katika kikao kazi kati ya wahariri, waandishi wa habari wa vyombo mbalimbali nchini chini ya uratibu wa Ofisi ya Msajili wa Hazina.

"Mikopo imewafikia wanufaika wapatao 183,381 kati yao wanawake 97,170 sawa na asilimia 53 na wanaume 86,211 sawa na asilimia 47."

Mfuko wa SELF (SELF MF) ni taasisi ya Serikali chini ya Wizara ya Fedha inayoshughulika na utoaji wa mikopo kwa wananchi hasa wa kipato cha chini wanaojishughulisha na shughuli za uzalishaji mali ili waweze kujiongezea kipato na kupunguza umasikini.

Mfuko wa SELF ulianza kutekeleza majukumu yake tarehe Mosi Julai, 2015, ukirithi majukumu ya Mradi wa Serikali uliojulikana kama “Small Entrepreneurs Loan Facility (SELF) Project. Mradi ulitekelezwa kwa kipindi cha miaka 15 kuanzia mwaka 2000 hadi 2015.

Vilevile, Afisa Mtendaji Mkuu huyo amesema, ili kutimiza majukumu ya mfuko huo kwa ufanisi wamejiwekea malengo makuu matatu katika mpango mkakati wake.

Mosi amesema ni kuwafikia wateja wengi zaidi hasa wa kipato cha chini na kutoa elimu ya fedha.

"Katika kipindi cha miaka mitano (2026-2030),mfuko unapanga kutoa mikopo kiasi cha shilingi bilioni 300 na kuwafikia wanufaika 200,000 na kuongeza matawi kutoka matawi 12 mpaka 22 kufikia 2030."

Pili,amesema mfuko umelenga kuongeza ufanisi ili kutoa huduma bora na kwa wakati. Amesema, hilo litawezekana kwa kubadilisha mifumo na kutumia zaidi teknolojia.

Jambo la tatu amesema, ni kuhusu uendelevu wa taasisi ambapo watasimamia utoaji wa huduma bora kuhakikisha mikopo inarejeshwa.

Pia, taasisi hiyo kuhakikisha inajiendesha kwa faida na huduma zinazotolewa zinakuwa endelevu nchini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news