NJOMBE-Mama Sanga anasema kuwa miaka mitatu iliyopita, alikuwa akiamka saa 10 alfajiri kila siku kwenda kuchota maji mtoni. Leo, anapofungua bomba lake la nyumbani saa 3 asubuhi, anatabasamu.
“Hata sijui kama ni ndoto au la,” anasema akiwa anaosha vyombo katika karo nyumbani kwake. “Kabla, kila nikitumia maji, nawaza namna nitakavyoyapata shida kuyapata tena yakiisha. Sasa hivi, hakika ninaishi mjini.” Mama Sanga anazungumza kwa bashasha.
Chanzo cha mradi wa maji (intake) wa Lugenge kinachotarajiwa kuongeza uzalishaji wa maji kwa Mji wa Njombe kiasi cha maji lita 1,440,000 kwa siku baada ya kukamilika kwa mradi huo.Mama Sanga ni miongoni mwa wakazi wapatao 70,168 wa Mji wa Njombe wanaonufaika na maboresho makubwa ya huduma ya maji yanayotekelezwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Njombe (NJUWASA).
Kwa sasa, huduma ya majisafi imefikia asilimia 76.4 ya wakazi wote 91,799 wanaoishi katika eneo la mamlaka hiyo kwa mujibu wa Sensa ya Taifa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 na makadirio ya sasa.
Kwa miaka mingi, Njombe ilikuwa ikikabiliwa na uhaba mkubwa wa maji. Mgao wa siku tatu kwa wiki ulikuwa jambo la kawaida, huku wananchi wakitegemea kununua maji au vyanzo vya asili.
Hali hiyo sasa imeanza kubadilika kwa kasi kupitia juhudi kubwa za NJUWASA chini ya uongozi wa Kaimu Mkurugenzi Mtendaji, Mhandisi Robert Lupoja.
Kwa sasa NJUWASA inatoa huduma ya maji kwa mgao katika baadhi ya maeneo. Hata hivyo, huduma ya maji imeanza kuimarika katika maeneo ya NSSF, Kilabuni, CCM, Melinze, Luhangano, Ngalanga, Nazareti, Airport, Mjimwema, Kilimani, Kihesa na Matamba.
Maeneo mingine 17 ya kihuduma yanapata maji kwa wastani wa saa 14 kwa siku. Lengo kuu ni kuwafikia wakazi wote kwa saa 24 na kuhakikisha huduma endelevu ya majisafi na salama kwa kila mwananchi.
NJUWASA inategemea vyanzo sita vya maji vya asili aina ya chemichemi, ambavyo ni Nyenga, Magoda, Lunyanywi, Wikichi, Kibena Howard na Ijunilo. Takwimu zinaonesha kuwa kati ya Julai 2024 hadi Machi 2025, mamlaka ilizalisha wastani wa lita milioni 5.3 za maji kwa siku na mahitaji halisi yakiwa ni lita milioni 10.4 kwa siku.
Hii ni sawa na upungufu wa asilimia 49. Lakini jitihada za kuziba pengo hilo zinaendelea kupitia utekelezaji wa miradi mipya, ukarabati wa vyanzo vya maji na upanuzi wa miundombinu ya usambazaji.
Mradi wa maji kutoka chanzo cha Ijunilo uliogharimu Shilingi bilioni 3.98 na tayari umeboresha hali ya upatikanaji wa maji katika mitaa Njombe Mjini, Livingstone na Kibena iliyopo katikati ya Mji wa Njombe
Pia, mradi wa maji kutoka chanzo cha Lugenge wenye thamani ya Shilingi bilioni 8.76, umefikia asilimia 84 ya utekelezaji.
Mradi huo unatarajiwa kuongeza uzalishaji kwa lita milioni 1.44 kwa siku na kuongeza muda wa upatikanaji wa maji kutoka saa 14 hadi 16 kwa siku na kuhudumia Maji katika Hospital ya Rufaa Mkoa wa Njombe pamoja na mitaa inayozunguka Hospitali ya Rufaa, Wikichi, Mgodechi, Ihege na Ramadhani iliyopo katika kata ya Ramadhani.
Mradi mkubwa zaidi ni wa Maji wa Miji 28, wenye thamani ya Shilingi bilioni 40.1, unaofadhiliwa kwa mkopo wa masharti nafuu kutoka Serikali ya India kupitia Exim Bank. Mradi huu unahusisha ujenzi wa mtambo mkubwa wa kutibu maji, banio (intake), pampu na mtandao wa mabomba.
Lengo kuu la mradi huu ni kupeleka huduma ya maji katika maeneo ya Hagafilo, Lunyanywi, Stendi Kuu Mpya ya Mabasi, Msete, Wende, Mjimwema na Ngalanga ukitarajiwa kukamilika Mei 2026.
Hata hivyo, NJUWASA inakabiliwa na changamoto ya upotevu wa maji unaokadiriwa kufikia asilimia 33, unaochangiwa na uchakavu wa miundombinu, uvujaji na wizi wa maji.
Ili kukabiliana na hilo, mamlaka imeanzisha ukarabati wa mtandao wa mabomba, ufungaji wa dira mpya za maji kwa wateja wapya, pamoja na uboreshaji wa mifumo ya TEHAMA iliyo rahisi kwa usomaji dira na ulipaji wa ankara kwa njia ya kidijiti.
Kwa sasa, NJUWASA inakusanya zaidi ya asilimia 92 ya malipo yanayotarajiwa kutoka kwa wateja wake.
Kwa upande wa jamii, mamlaka inaendeleza kampeni za uhamasishaji juu ya matumizi sahihi ya maji, ulipaji wa ankara kwa wakati, ulinzi wa vyanzo na miundombinu ya maji. Pia, imepanga kuanzisha huduma ya dharura ya maji kwa maeneo yanayokumbwa na changamoto za ghafla ili kuhakikisha huduma haisitishwi.
Kukamilika kwa miradi yote ya majisafi inayotekelezwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Njombe (NJUWASA) kunatarajiwa kuwa suluhisho la kudumu kwa changamoto ya upatikanaji wa huduma ya maji katika Manispaa ya Njombe.
Kwa kuongeza uwezo wa uzalishaji maji hadi lita 17,773,880 kwa siku kutoka lita milioni 5.3 za sasa, NJUWASA itakuwa na uwezo wa kukidhi mahitaji ya sasa na ya baadaye ya wakazi wa Mji wa Njombe.
Hali hiyo itaambatana na ongezeko la idadi ya wananchi watakaofikiwa na huduma kutoka asilimia 75.3 hadi zaidi ya asilimia 100, huku mtandao wa mabomba ukiongezwa na kuboreshwa ili kuwafikia wakazi wote.
Aidha, huduma ya maji itapatikana kwa saa 24 badala ya saa 14 kwa sasa, jambo ambalo linatarajiwa kuboresha maisha ya watu na kuchochea shughuli za kiuchumi katika maeneo yote yanayohudumiwa.