Rais Dkt.Samia atoa maagizo sekta za kilimo,mifugo na uvuvi

DODOMA-Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amewataka wananchi, Wizara na Taasisi zinazohusika na sekta za kilimo, mifugo na uvuvi kutumia kikamilifu miundombinu, teknolojia na mitaji iliyowekezwa na Serikali ili kuongeza tija na ushindani wa Taifa katika masoko ya ndani na nje.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akizindua Maabara Kuu ya Kisasa ya Kilimo iliyopo Mtumba jijini Dodoma tarehe 08 Agosti, 2025.
Akizungumza Agosti 8,2025 katika kilele cha Maonesho na Sherehe za wakulima, wafugaji na wavuvi (Nanenane) zilizofanyika kitaifa katika Viwanja vya Nzuguni, Rais Dkt. Samia amesema,miradi ya umwagiliaji iliyokamilika na inayoendelea kutekelezwa inapaswa kusimamiwa kwa viwango bora ili kuongeza eneo la kilimo cha umwagiliaji na kukuza tija ya mavuno.

Aidha, Rais Dkt. Samia ameeleza kuwa,Serikali ya Awamu ya Sita imeongeza bajeti ya kilimo ili kugharamia ujenzi na ukarabati wa skimu za umwagiliaji, mabwawa na visima,pamoja na kuanzisha mashamba makubwa ya pamoja, huku upatikanaji wa mbegu bora na mbolea ya kisasa ukiimarika kupitia ruzuku na kuanzishwa kwa viwanda vya uzalishaji,hatua iliyoongeza matumizi ya pembejeo nchini.

Ameongeza kuwa, ongezeko hilo la bajeti limewezesha miradi ya kimkakati chini ya Mpango wa Maendeleo ya Sekta ya Kilimo Awamu ya Tatu (ASDP III), huku Serikal ikiimarisha huduma za zana za kilimo na kuendelea kutoa ruzuku ya mbolea, sambamba
na kuhimiza elimu ya matumizi sahihi kwa wakulima.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akisikiliza maelezo kuhusu Maabara Kuu ya Kisasa ya Kilimo iliyopo Mtumba jijini Dodoma tarehe 08 Agosti, 2025.
Rais Dkt. Samia pia ameagiza maafisa ugani nchini kote kuendelea kutoa elimu ya matumizi ya pembejeo na kuhakikisha zana za kilimo zilizopo zinatunzwa vyema ili zitumike katika shughuli za uzalishaji.

Akizungumzia upatikanaji wa mitaji, Rais Dkt. Samia amesema, Serikali imewezesha sekta ya kilimo kwa kutoa mikopo yenye masharti nafuu na kuanzisha Benki ya Ushirika Tanzania yenye lengo la kusaidia wakulima, wafugaji na wavuvi kuwekeza kwenye miradi yenye mnyororo wa thamani.

Kuhusu Programu ya Jenga Kesho Iliyo Bora (BBT), Rais Dkt. Samia amesema,Serikali imeendelea kutenga maeneo makubwa ya uzalishaji kwa vijana na wanawake yenye zana za kisasa pamoja na kuwapatia mikopo ya riba nafuu ya uendeshaji.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu akielezea jambo baada ya kutembelea Maabara Kuu ya Kisasa ya Kilimo iliyopo Mtumba jijini Dodoma tarehe 08 Agosti, 2025.
Kuhusu sekta ya mifugo, Rais Dkt. Samia ameeleza kuwa Serikali imetenga ardhi kwa ajili ya malisho, imewezesha vijana kujiajiri kwenye ufugaji sambamba na kuzindua Kampeni ya Kitaifa ya Chanjo na Utambuzi wa Mifugo yenye lengo la kudhibiti magonjwa na kuongeza thamani ya mazao ya mifugo.

Kwa upande wa uvuvi, amesema Serikali inaendelea kutoa mikopo ya boti, vizimba na vifaa vya kisasa pamoja na uwekezaji katika Bandari ya Uvuvi ya Kilwa itakayoongeza ajira na kuimarisha shughuli za uvuvi wa bahari kuu.

Katika hatua nyingine, Rais Dkt. Samia amezindua Maabara Kuu ya Kilimo yenye viwango vya kimataifa, itakayokuwa kitovu cha maabara zote za kilimo nchini.

Maabara hiyo inajumuisha maabara ndogondogo 15 zenye uwezo wa kufanya uchunguzi wa mimea,wadudu, udongo, sumu kuvu, afya ya mimea na kuzalisha miche isiyo na magonjwa pamoja na kuboresha ubora wa mbegu.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akitembelea mabanda ya Maonesho ya Nanenane kujionea shughuli mbalimbali zinazoendelea katika viwanja vya Nanenane vilivyopo Nzuguni jijini Dodoma tarehe 08 Agosti, 2025.
Rais Dkt. Samia ameitaka maabara hiyo kujikita katika kazi za kisayansi na utafiti kwa umakini mkubwa, kwa kuzingatia kwamba jukumu hilo ndilo msingi wa usalama wa chakula wa Taifa, sambamba na kuagiza uanzishaji wa maabara maalum ya utafiti wa mbegu za asili, akisema hifadhi na utafiti wa mbegu hizo ni suala nyeti kwa mustakabali wa kilimo nchini.

Rais Dkt. Samia amesisitiza kuwa sekta za kilimo, mifugo na uvuvi ni nguzo za mageuzi ya
uchumi wa Taifa kwa mujibu wa Dira ya Maendeleo 2050 na Agenda 10/30 na kuahidi
kuendelea kuwekeza, kuwasikiliza wadau na kutumia TEHAMA ili kuongeza ushindani katika sekta hizo.
Matukio mbalimbali kwenye Maonesho ya Kitaifa na Kimataifa ya Nanenane, Nzuguni jijini Dodoma tarehe 08 Agosti, 2025.
Akirejea kaulimbiu ya maonesho ya Nanenane ya mwaka huu “Chagua Viongozi bora kwa Maendeleo Endelevu ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi 2025”, Rais Dkt. Samia amewahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi siku ya tarehe 29 Oktoba ili kushiriki Uchaguzi Mkuu na kusisitiza kuwa kuchagua viongozi bora ni nguzo ya maendeleo ya Taifa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news