Rais Dkt.Samia azindua Kituo cha Biashara na Usafirishaji Afrika Mashariki (EACLC)

DAR-Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan amesema, kukamilika kwa Kituo cha Biashara na Usafirishaji Afrika Mashariki (EACLC) kutawezesha kuzalisha ajira kwa vijana ambapo zaidi ya vijana 5,000 wamepata ajira za moja kwa moja,huku ajira 10,000 zaidi zikitarajiwa kuzalishwa wakati wa uendeshaji wa mradi huo.
Akizungumza Agosti Mosi,2025 wakati wa kuzindua kituo hicho kilichopo Ubungo, Dar es Salaam,Rais Dkt.Samia amesema,mradi huo utaifanya Tanzania kuwa chaguo la kwanza kwa wafanyabiashara na wasafirishaji wa bidhaa kutoka mataifa jirani na kuchochea ukuaji wa biashara ya kikanda na kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi katika Jumuiya ya Afrika Mashariki, COMESA, SADC na Eneo Huru la Biashara la Afrika (AfCFTA).
Kituo hicho kimejengwa kama sehemu ya juhudi za Serikali kuboresha mazingira ya biashara na usafirishaji, sambamba na Kongani ya Viwanda na Bandari kavu ya Kwala pamoja na kuanza rasmi kwa safari za mizigo kwa treni ya umeme ya SGR hapo jana.

Rais Dkt. Samia amesema,mradi wa EACLC ni wa kimkakati katika kutatua changamoto za biashara na usafirishaji zilizokuwa zikiikabili Tanzania na nchi jirani kwa muda mrefu, na kwamba kupitia kituo hiki, wafanyabiashara wa ndani na nje wataweza kufanikisha shughuli zao kwa ufanisi na gharama nafuu zaidi.
Ameongeza kuwa, kituo hicho kimewekewa mazingira wezeshi ya kuchochea mauzo ya
bidhaa za Tanzania nje ya nchi, hatua itakayosaidia kuongeza mapato ya Serikali, kukuza makusanyo ya Halmashauri na Manispaa ya Ubungo na kuongeza upatikanaji wa fedha za kigeni.

Rais Dkt. Samia pia amesema utekelezaji bora wa mradi huo unahitaji ushirikiano wa karibu
kati ya Serikali, sekta binafsi na wananchi, na kusisitiza kuwa Serikali itaendelea kuweka
mazingira rafiki kwa wawekezaji kupitia Mamlaka mpya ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi (TISEZA), ambayo itatekeleza dhana ya “One-Stop Centre” kwa ajili ya wawekezaji.

Aidha, Rais Dkt. Samia amewaalika wawekezaji wa ndani na nje kuchangamkia fursa zilizopo katika kituo hicho na amewasihi Watanzania kutumia fursa hizo kuanzisha au kukuza biashara zao na kuongeza thamani ya bidhaa katika soko la kikanda na kimataifa.
Katika kuhimiza uendelevu wa mradi huo, Rais Dkt. Samia ametoa rai kwa wawekezaji kuanzisha matawi ya kituo hicho katika maeneo mengine yenye shughuli nyingi za kibiashara nchini, akisisitiza kuwa hatua hiyo itasaidia kuongeza kasi ya ukuaji wa biashara, kuboresha mnyororo wa usambazaji na kuimarisha ushindani wa Tanzania katika masoko ya kikanda na kimataifa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news