DAR-Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB), Ibrahim Mwayela ametangaza rasmi kuanza kwa Ligi Kuu ya NBC msimu 2025/2026 inayotarajiwa kufungua pazia Septemba 17,2025 kwa michezo miwili itachezwa katika viwanja vya KMC, Dar es Salaam na Mkwakwani mkoani Tanga.
Akizungumza na waandishi wa habari Mwayela amesema kuwa maandalizi yote kuelekea kuanza kwa msimu mpya yapo tayari kwa upande wa usimamizi wa ligi Kuu ya NBC Pamoja na vilabu.
“Ligi Kuu ya NBC inarejea rasmi Septemba 17 ambapo siku hiyo kutakuwa na michezo miwili KMC itaikaribisha timu ya Dodoma Jiji katika uwanja wa KMC Complex na Coastal Union itakuwa mwenyeji wa timu ya Tanzania Prisons kwenye uwanja wa Mkwakwani,Tanga.
“Maandalizi yapo tayari kwa upande wetu kama Bodi ya Ligi na masuala yote ya usimamizi yapo vizuri huku klabu zote 16 zikiendelea kusajili ili kujiimarisha vema tayari kwa msimu mpya. Ratiba hiyo imezingatia matukio mbalimbali ya soka yaliyopo mbele yetu ikiwemo michuano ya kimataifa na kitaifa,” ameongeza Mwayela.
Mwayela amesema pamoja na hayo Ligi yetu inatarajiwa kutatamatika mei 23, 2026 ili kuruhusu wachezaji watakaopata nafasi ya kuitwa na timu zao zitakazofanikiwa kushiriki Kombe la Dunia mwaka 2026.
“Ligi inatarajiwa kutamatika Mei 23 ili kuruhusu wachezaji ambao timu zao za taifa zitafuzu Kombe la Dunia kwenda kujiandaa na michuano hiyo na mchezo wa watani wa jadi kati ya Young Africans na Simba ‘Kariakoo Dabi’ mzunguko wa kwanza utapigwa Disemba 13, 2025 huku mchezo wa marudiano ukipigwa Aprili 4,” amesema Mwayela.
Aidha, ameongeza kuwa ubora waliouonyesha wachezaji wa timu ya Taifa ya Tanzania katika michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani yaani CHAN umetokana na uimara wa Ligi Kuu ya NBC.
