Tuhakikishe vijana wanapata mafunzo ya ufundi stadi-Waziri Mkuu

LINDI-Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, ametoa wito kwa wazazi na walezi kote nchini kuhakikisha wanawapeleka vijana wao kupata mafunzo ya ufundi stadi yanayoratibiwa na Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) pamoja na Ofisi ya Waziri Mkuu ili kuwawezesha kupata ujuzi utakaowasaidia kujiajiri na kuchangia maendeleo ya Taifa.
Akizungumza mara baada ya kukagua karakana za kujifunzia zilizopo katika Chuo cha VETA wilayani Ruangwa mkoani Lindi, Waziri Mkuu alisisitiza kuwa Serikali imewekeza kwa kiasi kikubwa katika kuimarisha miundombinu ya vyuo vya ufundi stadi pamoja na kuratibu programu za mafunzo ili kuhakikisha vijana wanapata stadi zinazokidhi mahitaji ya soko la ajira la sasa na baadaye.

“Serikali inayo dhamira ya dhati ya kuhakikisha vijana wa Kitanzania wanakuwa na ujuzi. Mafunzo ya VETA na yale yanayotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu yanawawezesha vijana wetu kuajiriwa au kujiajiri wenyewe, na hii ni hatua kubwa ya maendeleo kwa familia zao na Taifa kwa ujumla,” alisema Waziri Mkuu.
Katika mazungumzo yake na baadhi ya wanafunzi alipokuwa akitembelea karakana chuoni hapo, Mheshimiwa Majaliwa alifurahishwa na namna ambavyo programu hizo za mafunzo zimekuwa na manufaa ya moja kwa moja kwa wanafunzi hao.

Kwa upande wake, Kaimu Mkuu wa Chuo hicho Mohamed Salum alisema kuwa VETA Ruangwa inaendelea kufanya maboresho mbalimbali kwa lengo la kupanua wigo wa kozi zinazotolewa ili kwenda sambamba na mahitaji ya soko la ajira. 

Alitaja jitihada zinazofanyika kuwa ni pamoja na mpango wa uanzishwaji wa fani mpya na uwekezaji katika vifaa vya kisasa vya kufundishia.
Naye Mwanafuzi mnufaika wa programu ya mafunzo ya Ofisi wa Waziri Mkuu, Maganga Salum amesema kuwa kabla ya kujiunga chuoni hapo hakuwa na ujuzi wowote, lakini kupitia mafunzo hayo sasa anaweza kufanya kazi za ufundi na ana matumaini makubwa ya kujiajiri mara baada ya kuhitimu. “Tumeiva na sasa tupo tayari kwenda kufanya kazi.”
Katika ziara hiyo, Waziri Mkuu pia alitembelea eneo linalojengwa hosteli kwa ajili ya timu ya mpira wa miguu ya Namungo sambamba na kukagua uwanja wa michezo wa Kassim Majaliwa uliopo Ruangwa ambao unatarajiwa kuwekwa viti katika majukwa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here