NA DIRAMAKINI
MWENYEKITI wa Kamati ya Kupambana na Rushwa ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SACC) ambaye pia ni Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Bw. Crispin Francis Chalamila amesema, mapambano dhidi ya rushwa yanahitaji ushiriki na ushirikishwaji thabiti wa wadau wote kutoka sekta zote.
Chalamila ameyabainisha hayo Agosti 4, 2025 wakati wa ufunguzi wa warsha ya Wakuu wa Taasisi za Kupamba na Rushwa za Ukanda wa SADC kuanzia Agosti 4 hadi 6,2025 jijini Arusha.Mgeni rasmi katika hafla hiyo alikuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Kassim Majaliwa kwa niaba ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan.
Warsha hiyo imeambatana na Sherehe za Maadhimisho ya miaka 20 ya Utekelezaji wa Itifaki ya SADC Dhidi ya Rushwa.
"Tunathamini sana mchango wenu katika mapambano dhidi ya rushwa. Kupambana na rushwa kunahitaji kujitolea kwa kila mtu na uwepo wenu hapa ni ushahidi wa kujitolea kwenu. Asanteni sana."Pia, amemshukuru Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), Mheshimiwa Elias Magosi ambaye amejumuika na washiriki wa warsha hii kwa njia ya mtandao.
"Tunapongeza juhudi hizi katika kuweka kasi na kuhakikisha kuwa nchi zote wanachama wa SADC zinakuwa sawa kuhusu maendeleo na hatua za utekelezaji wa Itifaki ya SADC Dhidi ya Rushwa."
Vilevile amesema kuwa, kupitia mikakati Miwili ya Kupambana na Rushwa ya (2018-2022) na (2023-2027),wamefanikiwa kuandaa mtaala wa Kikanda uliowekwa viwango vya uchunguzi na kinga dhidi ya rushwa.
Aidha,kuandaa Mfumo wa Ufuatiliaji na Tathmini wa Kikanda wa Kupambana na Rushwa pamoja na Kuandaliwa kwa Tathmini ya Kikanda ya Mapambano Dhidi ya Rushwa.
Pia, Bw.Chalamila amewashukuru washiriki wote katika warsha hiyo kutoka ndani na nje ya Tanzania huku akisisitiza kuwa,kupambana na vitendo vya rushwa kunahitaji kujitolea kwa nguvu zote.
Bw.Chalamila amesema,Itifaki ya SADC Dhidi ya Rushwa (The SADC Protocol Against Corruption) ilisainiwa Agosti 14,2001 mjini Blantyre, Malawi na ikaanza kutekelezwa mwaka 2005, hivyo ndiyo sababu kuu ya kuadhimisha miaka 20 ya utekelezaji wa Itifaki hiyo.
Amesema,kamati ndogo ya Kupambana na Rushwa SADC (SADC Anti-Corruption Committee-SACC) ilianzishwa kupitia kifungu cha 11 cha Itifaki ya SADC Dhidi ya Rushwa ambayo ilipitishwa mwaka 2001 na kuanza kutumika Julai, 2005.
"SACC ina jukumu la kusimamia utekelezaji wa Itifaki na kuandaa mikakati ya kupambana na rushwa ndani ya Kanda ya SADC."
Majukumu yake makuu ni pamoja na kukuza na kuimarisha mifumo ya kuzuia, kugundua, kuadhibu na kutokomeza rushwa katika sekta ya umma na binafsi, pamoja na kukuza ushirikiano kati ya nchi wanachama.
Kauli mbiu ya mkutano huu ni “Itifaki ya SADC Dhidi ya Rushwa @20-Kuwezesha Ushirikiano Endelevu wa Utangamano wa Kiuchumi, Amani, Usalama, na Utawala Bora katika Kanda ya SADC”.
"Kaulimbiu hii itaongeza thamani katika majadiliano katika warsha ya siku mbili. Warsha hii imeandaliwa mahususi kwa ajili ya wakuu wa mashirika ya kupambana na rushwa kutoka nchi wanachama wa SADC, pamoja na washirika na wadau husika kushiriki katika juhudi za kupambana na rushwa katika kanda na kwingineko."
Bw.Chalamila amesema, malengo mahsusi ya warsha hii ni kutafakari miaka 20 ya utekelezaji wa Itifaki ya SADC Dhidi ya Rushwa.
Lengo lingine ni kujadili maendeleo na changamoto zilizojitokeza tangu kuanza kutumika kwa Itifaki hiyo.
Vilevile, kutathmini mafanikio na kubaini mapungufu,kuelewa mafanikio yaliyopatikana na maeneo yanayohitaji maboresho katika sheria, uwezo wa taasisi, na ushirikiano wa kikanda
Aidha,kuweka vipaumbele vya kimkakati kwa siku zijazo na kufanya majadiliano ya kina kuhusu mustakabali wa itifaki hii kwa mtazamo wa muda mrefu.
Katika mkutano huu, Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Bw.Crispin Francis Chalamila, ambaye pia ndiye Mwenyekiti anayemaliza muda wake wa Kamati ya Kupambana na Rushwa ya SADC (SACC) tangu Oktoba 2024, atakabidhi rasmi Uenyekiti kwa kiongozi kutoka nchi ya Malawi.
Julai 21 hadi 25,2025 jijini Dar Es Salaam ulifanyika mkutano wa 27 wa Mawaziri wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama wa SADC (MCO) ambapo Tanzania ilipongezwa kwa kuonesha juhudi kubwa katika mapambano dhidi ya rushwa huku maeneo yenye nguvu yakiwa ni Mifumo ya kisheria.
Maeneo mengine ni dhamira ya kisiasa, na ushiriki wa wadau kwa kiwango kikubwa. Pongezi hizo zlitolewa na Katibu Mtendaji wa SADC, Elias Magosi kwenye ufunguzi wa mkutano huo.
Hivyo kupata pia heshima ya kuwa mwenyeji wa mkutano kwa mwaka huu ni uthibitisho wa nafasi ya Tanzania katika juhudi za Kimataifa za Kupambana na Rushwa.
TAKUKURU inatambua wajibu wake na imejipanga kuhakikisha kuwa maazimio ya mkutano huu yatachangia katika kuimarisha Utawala Bora, Amani na Maendeleo ya Kiuchumi ndani na nje ya mipaka yetu.









