TANGA-Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) imewahimiza wafanyabiashara, wamiliki wa kampuni na majina ya biashara jijini Tanga kuhakikisha wanasajili na kurasimisha shughuli zao ili kukuza uchumi wao binafsi na taifa kwa ujumla.
Wito huo umetolewa Agosti 14, 2025, na Kaimu Meneja wa Sehemu ya Majina ya Biashara chini ya Idara ya Makampuni na Majina ya Biashara kutoka BRELA, Bi. Subira Mwalumuli, wakati wa Kliniki ya Biashara inayoendelea katika viwanja vya Tangamano, jijini Tanga.
“Kama kauli mbiu yetu inavyosema, ‘BRELA ni Lango la Mafanikio ya Biashara Nchini’, basi ni muhimu kwa wananchi kutumia fursa hii kwa kupata huduma mbalimbali zinazotolewa na Wakala ili waweze kufikia mafanikio baada ya kurasimisha biashara zao,” alisisitiza Bi. Mwalumuli.
Aidha, alieleza kuwa BRELA inalenga kutatua changamoto zinazowakumba wafanyabiashara nchini, hususan katika eneo la usajili wa majina ya biashara na kampuni, kupitia kliniki za biashara zinazofanyika katika mikoa mbalimbali.
"Tunafahamu kuwa huduma zote za usajili kupitia BRELA zinapatikana mtandaoni kupitia Mfumo wa Usajili wa Mtandaoni (ORS-Online Registration System), lakini kuna wakati wafanyabiashara wanahitaji msaada wa ana kwa ana ili kuelewa taratibu zinazopaswa kufuatwa. Hii ndiyo sababu tunawatembelea na kutoa huduma za elimu na msaada zaidi," aliongeza.
Kwa upande wao, baadhi ya wafanyabiashara waliopata huduma katika kliniki hiyo wametoa pongezi kwa BRELA na kuomba kliniki hizo ziendelee kufanyika mara kwa mara, ili kutoa elimu na msaada kwa wafanyabiashara wadogo na wale wanaokumbwa na changamoto katika matumizi ya mfumo wa usajili.
"Huduma tulizopata hapa ni muhimu sana kwa sisi wafanyabiashara wadogo. Nilikuwa sijajua kabisa namna ya kusajili jina la biashara kwa njia ya mtandao, lakini kupitia maelekezo niliyopata leo nimeelewa hatua kwa hatua,” alisema Ally Waziri, mfanyabiashara wa mitumba kutoka maeneo ya Tangamano.Aliongeza kuwa elimu hiyo imemsaidia kuelewa umuhimu wa kuwa na biashara iliyo rasmi, hasa kwa ajili ya kupata fursa za kibiashara kama mikopo, tenda, na ushiriki katika maonyesho ya kitaifa na kimataifa.
Kliniki ya Biashara ya BRELA jijini Tanga inafanyika kwa siku tano ambapo ilianza tarehe 11 Agosti 2025 na inatarajia kuhitimishwa tarehe 15 Agosti, 2025 ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuwezesha mazingira wezeshi ya urasimishaji biashara.


