DAR-Waziri wa Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto, Mhe. Riziki Pembe Juma amesema ajenda ya Wanawake, Amani na Usalama ni matokeo ya Azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa Na. 1325 (2000) ambalo linazitaka nchi wanachama kuandaa na kutekeleza mipango ya Kitaifa kwa ajili ya kuhakikisha wanawake wanashiriki kikamikifu katika nyanja zote za amani na usalama.
Mhe. Riziki ameyasema hayo leo katika Uzinduzi wa Mpango kazi wa Kitaifa wa Kutekeleza ajenda ya Wanawake, Amani na Usalama 2025-2029 katika Ukumbi wa Chuo cha Mafunzo ya Ulinzi wa Amani Tanzania, Kunduchi jijini Dar es Salaam, wakati akitoa salamu za Zanzibar juu ya ushiriki wake katika uandaaji wa Mpango kazi wa Kitaifa wa Kutekeleza ajenda ya Wanawake, Amani na Usalama 2025-2029.
Amesema,Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) Kupitia Sera na Mipango mbali mbali, imetekeleza ajenda hiyo kwa vitendo katika nyanja mbali mbali ikiwemo ushiriki wa wanawake katika uongozi na kuongoza katika nafasi muhimu Serikalini.
“Sheria mbalimbali ikiwemo Sheria ya Mtoto Namba 6 ya mwaka 2011, Sheria ya Kumlinda Mwari na Mtoto wa mzazi mmoja ya mwaka (2004) na Sera ya Jinsia ya mwaka (2016) pamoja na uzingatiaji wa bajeti kwa Wizara zote 18 za Zanzibar ili kustawisha usawa wa kijinsia pamoja na kutunza maslahi bora ya Wanawake na Watoto SMZ Imetekeleza kwa vitendo,”amesema Pembe.
Pia, amesema wizara hiyo imetengeneza na kuzindua Mpango wa Kitaifa wa Kupambana na Vitendo vya Ukatili na Udhalilishaji wa Kijinsia (NPA-VAWC II 2025-2030) dhidi ya Wanawake na Watoto.
Ameeleza katika maandalizi ya Mpango kazi huo, Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto imeshiriki kikamilifu, hivyo amewaomba wadau wote Kutekeleza kwa vitendo ajenda za mpango kazi huo badala ya kubaki kuwa katika makaratasi.
Aidha,Mhe.Riziki ameshukuru ushirikiano unaondelea kati ya wizara anayoisimamia na Wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wanawake na Makundi Maalumu ya Tanzanzia Bara pamoja na kuomba mashirikiano hayo kuzidi kuendelea kwa lengo la kuleta Maendeleo katika Taifa.Uzinduzi wa Mpango kazi wa Kitaifa wa Kutekeleza ajenda ya Wanawake Amani na Usalama 2025-2029, umezinduliwa na Mhe. Dkt. Doto Mashaka Biteko, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, ambapo viongozi mbali mbali wa Kitaifa pamoja na viongozi wa Mashirika mbali mbali ya Ndani na nje ya nchi wamehudhuria.


